Kampuni za majani chai kuanza kutozwa ada mpya
TOM MATOKE na BARNABAS BII
KAMPUNI za kimataifa za majani chai nchini zitahitajika kulipa karibu Sh10,000 kwa kila ekari ya ardhi kila mwaka baada ya Tume ya Kitaifa ya Ardhi kutoa masharti mapya kuhusu umiliki wa ardhi kwa raia wa kigeni.
Serikali za kaunti katika maeneo ya upandaji majani chai zimekuwa zikishauriana na makampuni hayo kuhusu jinsi ya kutekeleza ada hizo kufuatia kupitishwa kwa katiba mpya mwaka wa 2010.
Kulingana na Waziri wa Kilimo katika Kaunti ya Nandi, Dkt Kiplimo Lagat, ada hizo mpya zitahitajika kuanza kutekelezwa Julai mwaka huu.
Kwenye gazeti la kitaifa lililochapishwa Machi 1, NLC iliagiza makampuni mbalimbali ya majani chai kutimiza masharti tofauti la sivyo hayatasajiliwa upya kukodisha ardhi.
Dkt Lagat alisema: “Kaunti zinashauriana na kampuni za kimataifa za majani chai katika maeneo ya Rift Valley na eneo la Kati ili kuamua kiasi ambacho makampuni yatastahili kulipa kama kodi ya ardhi bila kudhulumu kampuni hizo ambazo ndizo wawekezaji wakubwa wenye idadi kubwa ya wakazi walioajiriwa.”
Kampuni hizo zinapatikana katika Kaunti za Kericho, Bomet, Nandi na Kiambu.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Chama cha Wakuzaji Majani Chai Kenya, Bw Apollo Kairi alithibitisha kujitolea kwa wanachama wake kutimiza masharti hayo na pia kufuata mahitaji ya kikatiba.
Alisema hatua iliyochukuliwa itawezesha wawekezaji kuongeza muda wa kutumia ardhi zao kwa miaka 99 kuanzia wakati katiba mpya ilipopitishwa Agosti 27, 2010.
Kulingana na Dkt Lagat, Kaunti ya Kericho itakuwa ikitoza Sh10,000 kwa kila ekari kila mwaka huku Kaunti za Nandi na Bomet zikiendelea kushauriana na kampuni hizo kuhusu ada mpya zitakazotozwa.
Gavana wa Nandi, Bw Stephen Sang alisema wiki iliyopita kwamba wameongeza ada zao kutoka Sh100 hadi Sh5,000 kwa kila ekari kila mwaka.
Alilalamika kuhusu kampuni za majani chai ambazo hazijajitolea kuchangia kwa shughuli zinazonufaisha maisha ya wakazi kiuchumi na kijamii.
“Jamii ya Wanandi ilipoteza zaidi ya ekari 150,000 ya ardhi kwa upandaji wa majani chai na wanahitaji kusaidiwa kupitia uanzishaji wa miradi muhimu,” akasema Bw Sang.