Uchunguzi wa BBC wadai China inavua samaki Afrika kiharamu
Na MASHIRIKA
UCHUNGUZI wa shirika la habari la BBC umedhihirisha kuwa China imekuwa ikitumia mbinu haramu kuvua samaki katika Bahari ya Atlantic, ndani ya mipaka ya Siera Leone na mataifa mengine ya magharibi mwa Afrika.
Hatua hiyo imeharibu mazingira na kusababisha upungufu mkubwa wa samaki taifa hilo.
Kulingana na uchunguzi wa shirika hilo, meli za China zimekuwa zikivua samaki zikiwa mbilimbili kwa kuweka wavu mkubwa katikati, jambo ambalo ni haramu Siera Leone.
Shirika hilo lilionyesha, kwa kufuatilia kupitia mitambo ya Setilaiti jinsi meli hizo hutega wavu takriban mita 400 na kuvua samaki, kisha kuwauza kote duniani, haswa mataifa ya bara Uropa.
China inaripotiwa kuwa na meli za uvuvi kote duniani, huku pingamizi zikizidi kuibuka, raia wakiteta kuwa wanaachwa bila cha kuvua, huku wakizongwa na umaskini.
Wataalamu aidha wameeleza wasiwasi wao kuhusu hali hiyo, wakisema inaharibu mazingira.
“Mara tu mazingira yakishaharibiwa namna inavyoendelea, haitawezekana kuyarejesha namna yalivyokua,” Bw Percy Showers, mtaalam wa masuala ya uvuvi akaeleza.
Raia waomba msaada
Japo taifa hilo maskini kwa miongo kadhaa limepambana na vita vya kisiasa na ugonjwa wa Ebola miaka ya majuzi, tatizo la wavuvi kutoka China sasa linaibuka kuwa janga ambalo raia wanalia wasaidiwe.
“Hatufurahii hivi kwa kuwa sisi tunaachwa na samaki wachache sana wa kuvua. Tungependa serikali iwaondoe hawa watu waache kuvua katika nchi yetu,” akasema Abu Baki, ambaye ni mvuvi.
Kati ya meli zote zinazovua samaki katika mataifa ya Afrika Magharibi, robo tatu ni ya kutoka China, huku zingine zikiwa za kutoka Urusi na Bara Uropa.
Japo meli za Wachina huandamana na maafisa wa serikali ya Siera Leone, maafisa hao wanaripotiwa kulipwa mishahara duni, hivi kwamba hawana uwezo wa kuzungumza wanaposhuhudia vitendo haramu.
Hata hivyo, Waziri Emma Kowa, ameahidi kuchukua hatua akibaini kuwa meli hizo zinavunja sheria.
Na punde tu baada ya hakikisho lake meli kadhaa za China zilizuiwa kuvua kufuatia hali ya uchafu mwingi kwenye meli hizo, ambao unaweza kusababisha magonjwa.
Meli za China zinaripotiwa kuvua kati ya tani 60 na 100 za samaki kila siku nchini Siera Leone.
Suala la samaki wa kutoka China ambao wanauzwa mataifa ya Afrika Mashariki limekuwa likizua mizozo kutokana na hali yao kuwa wa bei rahisi na kumaliza wanabiashara wa mataifa haya.