• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 2:10 PM
Mwanasiasa, chifu matatani kwa uharibifu wa msitu Murang’a

Mwanasiasa, chifu matatani kwa uharibifu wa msitu Murang’a

Na SAMMY WAWERU

POLISI Murang’a wanachunguza mwanasiasa anayehudumu katika bunge la kaunti hiyo, wasaidizi wake wawili na ambao walikamatwa Jumanne, OCS na chifu kwa ukataji wa miti kiholela katika msitu wa serikali.

Kulingana na Kamishna wa Murang’a Mohammed Barre, mwanasiasa huyo anadaiwa kushirikiana na OCS, chifu pamoja na mfanyabiashara wa kibinafsi wa miti kuvuna karibu futi 10, 000 za miti katika Msitu wa Kahumbu, iliyopandwa katika ekari 20.

Bw Bare alisema miti hiyo inakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh700, 000.

“Imethibitishwa washukiwa hao wanachunguzwa kwa madai ya ukataji wa miti kinyume cha sheria, katika msitu huo ulioko kaunti ndogo ya Kigumo. Walitumia mashine sita za msumeno zinazomilikiwa na mfanyabiashara huyo. Operesheni ya kutafuta waliotumiwa kutekeleza uhalifu wa miti imeanza,” alisema.

Alisema maafisa wa usalama wamewapokonya miti hiyo na imehifadhiwa katika kituo cha polisi kama ushahidi.

“Tunaandaa ripoti kuhusu tukio hili, ambapo wahusika wanarekodi taarifa. Walioshuhudia pia wanarekodi taarifa kwa mujibu wa sheria, ili washukiwa wawasilishwe kortini,” akasema.

Alisisitiza kuwa sharti sheria ichukue mkondo wake, akionya kupiga kalamu yeyote atakayepatikana na hatia.

“Haiwezekani uwe serikalini ilhali unashirikiana na wanasiasa watundu na wafanyabiashara wenye tamaa za ubinafsi kuharibu maliasili yetu. Uhuni wa aina hiyo lazima ukomeshwe,” kamishna huyo alionya.

Alitaja washukiwa wote kama “wakiukaji wakuu wa sheria” akihoji katika siku za hivi karibuni wamehusika katika visa vya uhalifu kama ufisadi, ukataji wa miti na kushirikiana na waovu kuchoma shule eneo hilo.

Alisema njama ya kukata miti ilipangwa kupitia barua iliyoghushiwa, kinaya kikiwa inavyokashifu uharibu wa miti eneo hilo.

“Mmoja wa wasaidizi wa mwanasiasa huyo alijihami kwa barua iliyoruhusu miti kukatwa. Ilikuwa ghushi na ilieleza kwamba serikali ya kaunti ya Murang’a inahitaji miti kuunda shule ya umma,” Barre amesema.

Shule

Serikali za kaunti hazina jukumu lolote kuunda shule za umma kwa kuwa sekta ya elimu haijagatuliwa kupitia katiba ya sasa, na Kamishna Barre amesema maafisa wake watachunguza kisa hicho kwa kina na kwamba wote waliohusika kuharibu msitu wa umma lazima wafikishwe kortini.

Amesisitiza kuwa marufuku ya kitaifa ya ukataji wa miti katika misitu ya umma ni ya hadi Novemba 24, 2019, serikali ikiwa ndiyo yenye uwezo wa kuiondoa au kuiendeleza.

Februari 2018, Waziri wa Mazingira, Keriako Tobiko alitangaza marufuku hiyo kufuatia kilio cha umma kwa ukataji wa miti uliolaumiwa kusababisha maji ya mito kupungua nchini na hata mingine kukauka.

“Itaruhusu kuhamasisha kampeni ya upanzi wa miti, unaolenga kuafikia kigezo cha asilimia 10 ya misitu yetu kufikia mwaka wa 2022,” alisema Tobiko.

Waziri alisema bajeti ya Sh18 bilioni iliandaliwa ili kufanikisha upanzi wa miti kwa muda wa miaka mitano ijayo, Rais akawasilishiwa kwa minajili ya ufadhili.

Tangu marufuku ianze kutekelezwa ujenzi wa bidhaa za mbao umekuwa ghali, miti na vikingi vikiwa haba.

You can share this post!

Jeraha la Ronaldo pigo kwa Juventus

Wakazi wa Thika wahamasishwa jinsi wanavyoweza kutumia...

adminleo