Habari MsetoSiasa

Uhuru amfuata Ruto afisini

March 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

Rais Uhuru Kenyatta, jana alimtembelea Naibu Wake William Ruto katika afisi yake katika kile ambacho wadadisi wanasema ni juhudi za kutuliza joto la kisiasa nchini.

Rais Kenyatta alifika katika afisi ya Bw Ruto kwenye jumba la Harambee House Annex kwenye barabara ya Harambee mwendo wa saa saba mchana siku moja baada ya malumbano kuchacha ndani ya chama cha Jubilee na nchi kwa jumla.

Ujumbe kutoka Ikulu ulisema kwamba, viongozi hao wawili walikutana kwa chakula cha mchana na kujadili masuala yanayohusu ajenda za maendeleo ya serikali.

“Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake Dkt William Rut leo walishiriki chakula cha mchana ya kikazi katika afisi ya Naibu Rais Harambee House Annex, Nairobi ambapo viongozi hao wawili walijadili masuala yanayohusu ajenda ya maendeleo ya serikali,” ulisema ujumbe kutoka ikulu.

Wawili hao walikutana wakati ambao chama cha Jubilee kimegawanyika huku makundi mawili yakilumbana vikali kuhusu vita dhidi ya ufisadi na siasa za uchaguzi wa 2022.

Kundi moja linalomuunga Dkt Ruto linapinga muafaka kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, vita dhidi ya ufisadi na juhudi za kuleta uwiano nchini chini ya muafaka huo.

Wadadisi wanasema Rais Kenyatta alilenga kudhihirisha kwamba hajamtenga Naibu wake serikalini au kumlenga katika vita dhidi ya ufisadi yeye ( Ruto) na wandani wake wanavyodai.

“Kila hatua ambayo rais wa nchi anayochukua sio ajali, huwa imepangwa na inanuiwa kutimiza lengo fulani. Ikizingatiwa kwamba alimtembelea Naibu Rais wakati kuna msukosuko katika chama cha Jubilee, kuna ujumbe ambao alitaka kutuma kwa Wakenya kwamba hana kinyongo na Dkt Ruto kikazi,” alisema mdadisi wa kisiasa Tom Maosa.

Bw Ruto amekuwa akilaumu vita dhidi ya ufisadi akisema vimeingizwa siasa. Hasa, amekuwa akimtaja Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai, Bw George Kinoti kwa kutumiwa kisiasa kuvuruga ajenda yake ya kisiasa.

Wiki jana, Rais Kenyatta alisisitiza kuwa vita dhidi ya ufisadi havitamsaza yeyote hata akiwa mshirika wake wa karibu wa kisiasa, ndugu au dada yake, kauli ambayo wengi walichukulia alikuwa akimlenga Dkt Ruto.

Siku moja baadaye, wabunge wa Jubilee walilaumiana vikali kundi linalounga vita hivyo likimtaka Ruto kujiuzulu iwapo hafurahishwi na vita dhidi ya ufisadi.

Mnamo Jumatatu, seneta wa Siaya James Orengo ambaye ni mwandani wa Bw Odinga aliapa kuanza mipango ya kumtimua Bw Ruto afisini akidai amekiuka maadili.

Bw Ruto amekuwa akisisitiza kuwa Bw Odinga anatumia handisheki yake na rais kuvuruga mipango ya maendeleo ya serikali na upokezanaji wa mamlaka katika chama cha Jubilee.

Mwishoni mwa wiki, mgawanyiko katika chama cha Jubilee ulichacha wakati ambapo wabunge 12, wakiwemo tisa kutoka Jubilee, walipomlaumu Bw Ruto kwa kutomtii Rais Kenyatta na kumtaka ajiuzulu.