Habari MsetoSiasa

Mlima Kenya wapasuka vipande vitatu

March 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ERIC WAINAINA

MIGAWANYIKO zaidi inaendelea kujitokeza miongoni mwa viongozi wa kisiasa katika eneo la Kati, huku wote wakipania kuonekana kuwaunga mkono Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto.

Rais Kenyatta anahudumu kipindi chake cha mwisho, huku Dkt Ruto akilenga kumrithi mnamo 2022.

Tayari, kundi moja la viongozi linalojiita ‘Kieleweke’ limeungana kumlaumu Dkt Ruto kwa kupanga njama za kumzuia Rais Kenyatta kutimiza Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.

Kundi hilo linalilaumu kundi pinzani la ‘Tanga Tanga’ ambalo linamuunga mkono Dkt Ruto kwa kumsaliti rais, hasa kwenye kampeni yake dhidi ya ufisadi.

‘Tanga Tanga’ pia wanalaumiwa kwa kuwalinda watu wafisadi na kupinga juhudi za Rais Kenyatta kuiunganisha Kenya kupitia muafaka wake wa kisiasa na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Eneo hilo lina magavana watano, maseneta wanano, seneta mmoja maalumu, wabunge watano wawakilishi wa kike na wabunge 34 ambao wamebuni kundi la ‘Kieleweke’ linalomuunga mkono Rais Kenyatta.

Vile vile, kuna kundi la wanasiasa ambao hawajajiunga na makundi hayo mawili.

Kundi la ‘Tanga Tanga’ linawajumuisha Gavana Ferdinard Waititu (Kiambu), wabunge Faith Gitau (Nyandarua), Cate Waruguru (Laikipia), Wangui Ngirichi (Kirinyaga), Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Ndindi Nyoro (Kiharu), Patrick Wainaina (Thika Mjini), Jonah Mburu (Lari), Githua wa Machukuru (Kabete), Jeremiah Kioni (Ndaragwa), Mary Waithira (Maragwa), Alice Wahome (Kandara) Rigathi Gachagua (Mathira), John Kiarie (Dagoretti) na Charles Jaguar (Starehe).

Kundi hilo limekuwa likiandamana na Dk Ruto katika sehemu mbalimbali nchini, huku likidai Rais Kenyatta anamlenga kwenye vita vyake dhidi ya ufisadi.

Kundi la ‘Kieleweke’ ambalo linaongozwa na mbunge maalum Maina Kamanda linawajumuisha Seneta wa Nyeri Ephraim Maina, wabunge Isaac Mwaura, Gathoni wa Muchomba (Kiambu), Paul Koinange (Kiambaa), Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), Mercy Gakuya (Kasarani), Peter Mwathi (Limuru), Muturi Kigano (Kangema), Francis Waititu (Juja) na wabunge wengine waliohudumu awali.

Kundi hilo limekuwa likizuru makanisa katika maeneo ya Nairobi na Kati kumtetea Rais na ajenda zake za maendeleo. Wabunge hao vile vile wamekuwa wakiwalaumu wenzao kwa kumkosea heshima Rais Kenyatta na kupinga miradi yake ya maendeleo.

Waliosalia kimya

Hata hivyo, viongozi wengi katika eneo hilo wameamua kubaki kimya, huku maswali yakiendelea kuwepo kuhusu mrengo wanaoegemea.

Viongozi hao hata hivyo wamekuwa wakikwepa kuhudhuria hafla za Bw Ruto katika eneo hilo. Majuma mawili yaliyopita, Seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi na wabunge wanane walikosa kuhudhuria hafla moja alikokuwepo Dkt Ruto katika eneo la Kabete.

Badala yake, waliamua kuhudhuria ibada ya kanisa katika eneobunge jirani la Kikuyu.

Mwenyekiti wa Baraza la Jamii ya Agikuyu Wachira Kiago anasema ni dhahiri kwamba viongozi wengi katika ukanda huo wameacha kumuunga mkono Rais.

“Viongozi wengi katika eneo la Kati hawamtetei tena Rais Kenyatta. Hao ni watu wanaolenga kusambaratisha ajenda yake ya maendeleo,” akasema.