Habari MsetoSiasa

Hatuna haja na pesa, twataka mageuzi – Wakulima wa kahawa

March 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

WAKULIMA wa kahawa na washikadau wengine katika sekta hiyo, wamekosoa hatua ya serikali ya kuanzisha hazina ya Sh3 bilioni kuokoa kilimo cha kahawa wakisema wanataka mageuzi.

Japo Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuwa hazina hiyo itatumiwa kuwapa mikopo wakulima kwa riba ya chini, baadhi ya wadau wanahoji kuwa biashara ya kahawa imeanguka na hakuna haja itengewe pesa.

Badala yake wanataka tofauti ya malipo kwa zao la kahawa liangaziwe.

“Soko la kahawa limekuwa likipendelea mazao yanayokuzwa maeneo ya milimani kuliko ya maeneo ya chini, ya awali yakilipwa bei nzuri. Wakulima wa maeneo ya juu wanalipwa zaidi ya Sh100 kwa kilo lakini wa maeneo ya chini wanalia kuwa wanalipwa vibaya,” alisema Bw Daniel Miriti, afisa wa Muungano wa Wakulima wa Kahawa eneo la Mlima Kenya.

Bw Miriti alisema wanachohitaji wakulima wa mmea huo sasa ni kujengewa kiwanda cha kuchanganya kahawa ya maeneo ya milimani na inayokuzwa maeneo ya chini, kabla haijauzwa sokoni, ili kahawa ya Kenya iwe ikiuzwa nje ikiwa bora zaidi.

Alisema kutengenezwa kwa viwanda hivyo kutasaidia kahawa ya humu nchini kuchanganywa na kuundwa inavyohitajika sokoni, na hivyo kuwapa wakulima uwezo wa kuamua bei watakayouza.

“Tunataka kahawa ya maeneo ya milimani iwe ikichanganywa na ile ya maeneo ya chini humu nchini badala ya kuiuza ikiwa tofauti kisha inaenda kuchanganywa sokoni. Hivyo tutawasaidia wakulima wote, wa maeneo ya milimani na maeneo ya chini,” akasema.

Uzani wa chini wa kahawa inayouziwa viwanda vya kusaga kahawa pia umetajwa kuwa sababu nyingine ambayo imefanya malipo kwa wakulima kuwa duni.

Mshauri wa serikali ya Kaunti ya Murang’a kuhusu kilimo cha kahawa, Bw Paul Mutua alisema ikiwa viwanda vitawekeza kwa teknolojia ili kubaini kuwa kila kahawa inayopimwa na kuingia viwandani ni ya ubora unaohitajika, wakulima watapata faida zaidi na kulipwa Sh100 na hata zaidi kwa mazao wanayouzia viwanda.

“Nusu ya kahawa iliyouziwa viwanda mwaka wa 2017/18 haikuuzwa baada ya kukaguliwa, nusu ilikuwa imeharibika,” alisema Bw Mutua.

Afisa huyo alisema licha ya madai kuwa pesa za wakulima zinaibiwa sokoni, kuna wakulima wanaopeleka viwandani kahawa mbovu na ambayo haiwezi kuuzwa sokoni.

“Hii imefanya wengi kuanza kutupilia mbali kilimo cha kahawa na kuanza kukuza vitu vingine baada ya kufa moyo. Kwa miaka mitano iliyopita zaidi ya ekari 1,000 zilizokuwa zikikuzwa kahawa sasa zinafanyiwa vitu vingine,” akasema.

Kaunti ya Kirinyaga imekuwa mstari wa mbele kuanza kupigania wakulima wake, ikisema inapanga kufungua maduka ya zao hilo Uropa ili kuuzia wateja wake.