• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Matapeli wanavyotumia mazishi bandia kulaghai wabunge

Matapeli wanavyotumia mazishi bandia kulaghai wabunge

Na SAMWEL OWINO

WALAGHAI sasa wanatumia matanga feki kuwatapeli wabunge, imebainika.

Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kuwa wabunge wamekuwa wakitapeliwa na walaghai wanaotumia mazishi hewa na shida nyinginezo kama vile ugonjwa, gharama za hospitalini na karo.

Mnamo Februari 1, mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo alitumia mtandao wa Facebook kuelezea jinsi alivyohudhuria mazishi feki.

Familia ya mtu aliyedaiwa kufariki ilishtuka ilipomuona Bi Odhiambo akiwasili kuhudhuria mazishi ya mpendwa wao ambaye alikuwa hai.

“Kila mara mimi husimama na watu wa eneobunge langu wakati wa furaha na huzuni, haswa wakati wa mazishi ambayo hufanyika Alhamisi au Ijumaa. Leo nilikuwa na orodha ya mazishi ya watu 10.

“Lakini tulibaini kuwa mazishi ya watu wawili yalikuwa feki na ulikuwa utapeli ulioendeshwa na watu wanaotaka kujipatia fedha kwa njia za kilaghai,” akasema Bi Odhiambo.

Bi Odhiambo alielezea namna alivyotuma salamu za rambirambi kwa familia anayoifahamu kwa ‘kupoteza’ mwanao, lakini ikabainika kuwa ‘marehemu’ alikuwa buheri wa afya.

Uchunguzi wetu ulibaini kuwa walaghai hao hupendelea kutapeli wabunge wanaohudumu kipindi cha kwanza ambao wangali wanajitafutia umaarufu wa kisiasa.

Walaghai hao mara nyingine hushirikiana na mameneja wa Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (CDF) na kuongeza idadi ya mazishi kwa lengo la kunufaika na fedha zinazotumwa na mbunge kufariji familia zilizopoteza wapendwa wao.

“Mara nyingi wabunge wanapopata taarifa kuhusu matanga hupigia simu mameneja wa hazina ya CDF ili kuthibitisha. Walaghai hao hushirikiana nao kuongeza idadi ya matanga, ikiwa kuna hafla 10 za mazishi kwa wiki, mameneja husema watu 15 wamefariki ili waweze kunufaika na fedha za ziada,” anasema mbunge wa Kasipul, Bw Charles Were.

Mwakilishi wa Kike wa Kaunti anadaiwa kutapeliwa Sh700,000 miezi mitatu iliyopita na watu waliojifanya kwamba wamefiwa na wameshindwa kulipia gharama za matibabu hospitalini. Matapeli hao pia walihitaji msaada kwa ajili ya mazishi.

Japo mbunge huyo hakuwa na fedha wakati huo, alikopa kwa mwenzake na kuwatumia matapeli hao ambao walitoweka.

Mbunge huyo wa kaunti amekuwa akiona haya kufichua kuhusu kisa hicho

“Hataki kusema masaibu hayo, lakini mimi najua kwa sababu tunatoka naye kaunti moja,” mbunge aliyetaka jina lake libanwe akaambia Taifa Leo.

Mbunge wa Maragwa Mary Wamaua Waithera, alisema kuwa alitapeliwa Sh5,000 na mwanamke aliyedai kuwa mkurugenzi wa elimu wa Kaunti ya Murang’a.

Naye, Mbunge wa Mugirango Kaskazini, Bw Joash Nyamoko alisema kuwa alitapeliwa na watu waliompigia simu wakilia lakini ikabainika kwamba yalikuwa matanga bandia.

You can share this post!

Ni rahisi kwa wafisadi kuhalalisha mali ya wizi Kenya...

Mchakato wa uchaguzi wa mawakili warahisishwa

adminleo