Habari Mseto

Uganda ipewe ardhi lakini kwa mkataba maalum, makuli sasa wasema

April 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

Chama cha Makuli nchini kimemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuweka mkataba maalum na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni kabla ya kumpa ardhi humu nchini.

Wiki iliyopita Rais Kenyatta alisema atampa mwenzake wa Uganda ardhi eneo la Naivasha kujengea bandari (dry port) kuhifadhia mizigo yao kama mpango wa reli ya kisasa SGR kati ya nchi hizo mbili.

Hata hivyo wafanyikazi 7, 000 wa bandari ya Mombasa wana wasiwasi kuhusiana na mpango huo huku wakimtaka Rais Kenyatta kuhakikisha kuna mkataba kati yao.

Wakiongozwa na Katibu wa makuli nchini Bw Simon Sang wafanyikazi hao walisema wanaunga mkono hatua hiyo hata hivyo walimtaka Rais Kenyatta aweke mkataba na mwenzake ambao utalinda nchi zote mbili.

“Rais Kenyatta aweke mkataba mkali kabla ya kutoa ardhi kwa mwenzake wa Uganda. Mkataba huo unafaa uangalie maslahi ya nchi zote mbili kuwe na usawa na haki kati ya raia wote. Ardhi hiyo inatolewa vipi? Kila kitu kiwekwe paruwanja kwa manufaa ya Wakenya,” alisema Bw Sang.

Bw Sang alisema ni muhimu kwa wawekezaji kupewa ardhi lakini kuwe na mkataba maalum.

”Ajira ni mojawapo ya mkataba muhimu ambayo inafaa kunufaisha wakenya na waganda, hiyo ndio tunapigania,” Bw Sang alisisitiza.

Jumatano iliyopita kwenye ziara ya Bw Museveni humu nchini katika chajio ikulu ya Rais huko Mombasa, Bw Kenyatta alisema Kenya itaipa Uganda ardhi kujengea bandari.

Lakini kwenye kikao na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama cha makuli nchini huko Mombasa, Bw Sang alisisitiza kuwa makuli wanaunga mkono hatua ya Rais Kenyatta lakini walimtaka aweke mkataba na mwenzake wa Uganda ambapo Wakenya hawatonyanyaswa au kudhulumiwa.

Uganda ni soko kubwa zaidi katika bandari ya Mombasa nchi zengine zikiwa Congo, South Sudan na Rwanda.