TAHARIRI: Afisa aliyedhulumu wanahabari akamatwe
NA MHARIRI
MASHAMBULIZI dhidi ya wanahabari yameanza kuwa jambo la kawaida hapa nchini.
Kila mtu anayehisi kubanwa hukimbilia kuwatusi, kuwalaumu au hata kuwashambulia wanahabari. Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria, ni wa punde zaidi kuwashambulia wanahabari wa kampuni ya Nation Media Group kwenye mtandao wa Twitter, kwa kuwaita “watumwa wa mwajiri wao”.
Kisa na maana ni kuwa, gazeti la Sunday Nation lilichapisha kibonzo cha Bw Kuria akiwa ametokwa na ulimi mrefu na maandishi ‘Kijana wa zamani wa kanisa mwenye ulimi wa sumu.’
Mchoraji katuni na wahariri wa gazeti hilo wanaamini kuwa japokuwa Bw Kuria anadai kuwa aliwahi kuwa kijana wa kutumika madhabauni, tabia zake, matamshi yake na mienendo haviendi sawa na sifa hiyo.
Amekuwa akitoa cheche za matusi, kuwaombea wanasiasa wengine kifo n ahata wakati mmoja alimwita Kinara wa chama cha ODM, Raila Odinga majina yasiyochapishika na kudai angemfanyia kitendo fulani.
Naibu Kamishna wa Kaunti eneo la Miharati naye Ijumaa aliwashambulia wanahabari waliokuwa kazini wakati wa maandamano ya wakongwe. Aliwaamuru maafisa wa polisi wa Utawala wawapokonye wanahabari hao vifaa vyao vya kazi na kuhakikisha hawakurekodi matukio hayo.
Wanahabari hao wa runinga za Njata na Gikuyu walikuwa wakitekeleza wajibu wao wa kufahamisha umma kuhusu yaliyokuwa yakitokea.
Kifungu cha 35 cha Katiba kinaeleza haki ya umma kupata habari. Ukijumuisha na kifungu cha 33 kuhusu Uhuru wa Vyombo vya Habari, inasikitisha sana kuona Bw Kuria na Naibu huyo wa Kamishna wa Kaunti wakiwa wangali kazini.
Wizara ya Usalama wa Ndani imetangaza kuwa inachunguza madai dhidi ya Naibu wa Kamishna wa Kaunti. Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) inapaswa kujibu maswali kuhusu maafisa inaowaajiri kutumikia umma.
Kwa afisa huyo kutangaza kuwa hakuna mwanahabari atakayefanya kazi yake katika eneo analosimamia bila ya ruhusa yake, ni wazi haelewi katiba ya nchi hii inavyosema.
Afisa kama huyo anatumia vibaya afisi yake, jambo ambalo ni ukiukaji wa Sura ya Sita kuhusu Maadili. Inashangaza kuwa bado yupo kazini kufikia leo.