• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
Wabunge watishia kuchochea wakazi wajihami kwa silaha

Wabunge watishia kuchochea wakazi wajihami kwa silaha

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wanne kutoka Rift Valley, wametisha kuwachochea wakazi wa Elgeyo Marakwet kuchukua sheria mikononi mwao kwa kujihami kwa silaha ikiwa serikali haitadumisha usalama katika eneo hilo.

Wakihutubia wanahabari Jumanne katika majengo ya bunge, Nairobi wabunge; Kagongo Bowen (Marakwet Mashariki), William Kisang (Marakwet Magharibi), Wilson Sossion (Mbunge Maalum) na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet Jane Chebaibai Kiptoo walisema wakazi wa eneo hilo wamechoshwa na uvamizi wa kila mara unaotekelezwa na wahalifu kutoka eneobunge la Tiaty.

“Mnamo Jumapili wanafunzi wawili wa shule ya msingi ya Chesawach katika eneobunge la Marakwet waliuawa kinyama kwa kupigwa risasi na wavamizi kutoka jamii ya Wapokot. Je, wavulana hawa, Colins Kiprono (9) na Aaron Kiprono (10) walifanya kosa gani ndipo wakauwa kikatili jinsi hiyo,” akauliza Bw Bowen.

“Ikiwa serikali haiwahakikishii usalama watu wetu wanaoishi eneo la Bonde la Kerio, basi pia hatutakuwa na jingine ila kuwauliza wajihami kwa bunduki ili wajikinge,” akaongeza mbunge huyo wa chama cha Jubilee.

Naye Bw Kisang alimtaka Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i kuzuru eneo hilo ili kushuhudia namna ambavyo shughuli za masomo zimeathirika baada ya kuzorota kwa hali ya usalama.

“Kufuatia kisa cha Jumapili ni shule mbili pekee zingali zinaendelea na masomo katika eneobunge la Marakwet Mashariki. Shule zingine zote zimesalia mahame huku walimu wasio wenyeji wakitorokea usalama wao. Hatuwezi kuvumilia hali kama hii,” akasema Bw Kisang.

Bw Sossion alisema walimu hawakubali kufanya kazi kama maeneo ambako utovu wa usalama umekithiri endapo serikali haitachukua hatua zifaazo kurejesha usalama.

Mwaka jana zaidi ya walimu 500 na walimu kutoka shule zilizoko karibu na mpaka wa Tiaty na Marakwet Mashariki walihamia maeneo salama baada ya mapigano kuzuka.

You can share this post!

TAHARIRI: Huduma Namba ina manufaa tele

GWIJI WA WIKI: Justus Kyalo Muusya

adminleo