Habari Mseto

Mawakala bondeni wapunja wakuzaji mahindi mamilioni

April 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BARNABAS BII

WAKULIMA wa mahindi katika ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa wamepoteza mamilioni ya pesa kwa mawakala walaghai ambao hununua mahindi kwa ahadi ya kuwalipa lakini wanatoweka na pesa zao.

Maafisa wa usalama katika eneo hilo wamemkamata mwanamume anayeaminika kuwa mshukiwa mkuu wa mtandao huo, baada ya malalamishi kutoka kwa wakulima. Wakulima hao wanakisiwa kupoteza karibu magunia milioni moja ya mahindi.

Mmoja wa washukiwa hao alikamatwa katika eneo la Ziwa, Kaunti ya Uasin Gishu baada ya kuwalaghai wakulima magunia zaidi ya 700. Alikuwa akiahidi kuwalipa Sh3,000 kwa kila gunia, kinyume na bei ya Sh2,500 inayotolewa na Halmashauri ya Kitaifa ya Ununuzi wa Nafaka (NCPB).

“Walaghai hao wanawahadaa wakulima kwa kuwaahidi kwamba watawalipa Sh3,000 kwa kila gunia kwa muda wa wiki moja,” akasema Mkuu wa Polisi wa Eldoret Magharib, Zacharia Bitok.

Alisema washukiwa wengine watatu wamekamatwa kuhusiana na sakata hiyo, ambapo wakulima wanakisiwa kupoteza mamilioni ya pesa.

“Watu hao huwa wanaendesha shughuli zao katika maeneo mbalimbali ya ukanda huu. Wamefungua vituo mbalimbali vya kununulia mahindi na wanaaminika kuwa na ushirikiano wa karibu na baadhi ya wafanyakazi wa mashirika ya utoaji misaada,” akasema Bw Bitok.

Kutokana na hayo, Chama cha Kitaifa cha Wakulima (KFA) kimewatahadharisha wakulima kuwa waangalifu dhidi ya kuporwa na walaghai hao.

“Wakulima wengi watapunjwa ikiwa hawatachukua tahadhari za kutosha. Wanapaswa kuuza mazao yao kwa NCPB, wasagaji na wafanyabiashara halali,” akasema mkurugenzi mkuu wa chama hicho Kipkorir Menjo.