• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Rais apuuza njaa na kupanda kwa gharama ya maisha

Rais apuuza njaa na kupanda kwa gharama ya maisha

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Alhamisi alikwepa kuzungumzia suala la njaa nchini pamoja na kupanda kwa gharama ya maisha, alipohutubia Bunge jana kuhusu hali ya taifa.

Wabunge kutoka maeneo kame walimkosoa Rais kwa kupuuza masuala hayo yanayomhusu mwananchi wa kawaida, wakisema walikuwa na matarajio makubwa kwamba angetangaza mikakati ya serikali yake katika kupambana na janga hilo, ambalo limesababisha maafa katika maeneo kadhaa nchini.

“Tulitarajia Rais kuelezea mikakati ambayo serikali yake imeweka kupambana na njaa na kiangazi, ambacho kimeathiri watu wetu na mifugo. Tunasikitika kuwa hakutaja suala hilo kwenye hotuba yake,” akasema Mbunge wa Turkana Mashariki, Nakara Lodepe.

Mbunge wa Kiminini, Chris Wamalwa naye alimkosa Rais akisema hawezi kusema kuwa taifa liko katika hali nzuri, ilhali ni majuzi tu ambapo watu kadhaa waliripotiwa kufariki kutokana na njaa katika Kaunti za Baringo na Turkana.

“Nadhani Rais angeelezea mikakati ambayo serikali yake imewaka kukabiliana na hali ambayo inachangiwa na usimamizi mbaya wa rasimali za umma,” akaeleza.

Kauli sawa na hiyo ilitolewa na wabunge Mugambi Rindikiri (Buuri), William Kamket (Tiaty) na Martin Owino (Ndhiwa).

Mapema mwezi jana, takriban watu 11 waliripotiwa kufariki katika eneo bunge la Tiaty, Kaunti ya Baringo katika kile ambacho kilisemekana ni maradhi yanayosababishwa na njaa. Hata hivyo, maafisa wakuu wa serikali wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto walikanusha habari hizo.

Katika hutuba yake jana Rais Kenyatta pia hakusema lolote kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha. Hii ni licha ya takwimu kutoka Benki Kuu (CBK) kuonyesha kuwa katika kipindi cha mieizi miwili iliyopita, mfumko wa bei umepanda kwa asilimia 4.

Hii ni kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa za mafuta na vyakula kama vile unga wa mahindi, ambao sasa unauzwa kwa bei ya wastani wa Sh90 kwa pakiti moja ya kilo mbili, kutoka bei ya Sh75 mwezi Februari.

You can share this post!

Katu sitaacha kutangatanga, asema Ruto

Upinzani waunga Rais mkono katika vita dhidi ya ufisadi

adminleo