ODM yakubali kushindwa Ugenya, Embakasi Kusini
Na CHARLES WASONGA
HATIMAYE chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kimekubali kushindwa katika chaguzi ndogo zilizofanyika katika maeneobunge ya Ugenya na Embakasi Kusini.
Mkurugenzi wa uchaguzi katika chama hicho Junet Mohammed, kwenye taarifa, amesema kwamba ODM inachunguza kiini cha kushindwa kwa lengo la kubaini ikiwa wanaendesha shughuli hizo kwa njia ambayo inahitaji kufanyiwa ‘marekebisho’.
“Tutaketi kama chama kubaini kile ambacho kilienda visivyo na kusababisha wagombea wetu kushindwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa makosa hayo hayarejelewi tena,” akasema Bw Mohammed ambaye ni Mbunge wa Suna Mashariki.
Mbunge huyo pia alimshukuru kiongozi wa Jubilee Rais Uhuru Kenyatta kwa kutowasilisha wagombea katika chaguzi hizo, akisema huo ulikuwa uamuzi wa busara uliogeuza chaguzi hizo kuwa mashindano kati ya vyama ndugu chini ya muungano wa Nasa.
“Tunamshukuru kiongozi wa Jubilee Rais Uhuru Kenyatta ambaye katika moyo wa handisheki, aliamuru chama chake kujiondoa katika chaguzi ndogo za Ugenya na Embakasi Kusini. Uamuzi huo uligeuza chaguzi hizo kuwa ushindani kati ya wandani na vyama shirika,” Mohammed akasema.
Kulingana na mbunge huyo, chaguzi hizo mbili ziliashiria siasa za kuvumiliana huku akiwapongeza walioshiriki.
“Katika mashindano hayo mawili, wapigakura wameelezea kuwa wanathamini siasa za kuvumiliana, na kuendeleza ajenda za kitaifa. Tunapongeza hali hii kwani inalandana na sera ya chama chetu na ambacho tunalenga kuendelea kupitia muafaka ambao Rais Kenyatta na kiongozi wetu Raila Odinga walitia saini mnamo Machi 9, 2019,” akasema.
ODM iliwapongeza washindi na wapigakura na wagombeaji wote kwa kuendesha shughuli zao kwa heshima katika kipindi chote cha kampeni na baada ya kutangazwa kwa matokeo.