Habari Mseto

Makahaba waililia serikali iwasaidie kuwekeza wakomeshe biashara ya uzinzi

April 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

ERICK MATARA NA RICHARD MAOSI

MAKAHABA 14 mjini Nakuru wameiomba serikali ya kaunti na wahisani kujitokeza ili wawasaidie kuachana na biashara ya kuuza miili yao.

Wakizungumza na Taifa Leo Dijitali, walihakikishia umma kwamba walikuwa tayari kuachana na ukahaba na kutafuta njia mbadala ya kujipatia mapato iwapo watapewa msaada kuwekeza kwa biashara.

Kwa mujibu wa msemaji wao Martha (sio jina lake halisi),  wameanzisha mfumo wa mageuzi wakitarajia kubadilisha mienendo siku za hivi karibuni.

“Tunakusudia kunyoosha mienendo na kuachana na ukahaba, isipokuwa changamoto inayotukabili ni ukosefu wa mtaji wa kuanzisha biashara,” alisema.

Baadhi yao waliungama kuwa alijiingiza kwenye biashara ya ngono kwa sababu ya ukosefu wa ajira, kukidhi maslahi ya watoto wake tano.

Walipokosa namna ya kukidhi mahitaji ya familia, hawakuwa na budi kujitosa ndani ya ukahaba.

“Sio nia yetu kuhangaika barabarani kila siku, kusema kweli tumekubali kwa sauti moja kuachana na ukahaba mradi tu wasamaria wema wajitokeze kutusaidia,” walisema.

Makahaba katika eneo la Three Ways katikati ya mji wa Nakuru wakisaka wateja kwa bidii gizani. Picha/ Richard Maosi

Mwaka 2018, mwenyekiti wa Muungano wa Wafanyibiashara Nakuru, Muchemi Mwangi alilalamika aliposema changudoa walikuwa wakitatiza shughuli za kibiashara na kuwatorosha wawekezaji .

Aidha wateja walianza kununua bidhaa kwingine, pale makahaba walipoanza kujazana mbele ya maduka ya kuuzia.

Ikizingatiwa kuwa kaunti ya Nakuru inatarajiwa kufikia hadhi ya kuwa jiji karibuni, makahaba wameanza kumiminika mjini na kutatiza shughuli za kibiashara.

Wakati mwingine wasichana wenye umri mdogo hupiga foleni ndefu mbele ya maduka na kwahangaisha wauzaji wanaowahudumia wateja.

Maeneo yaliyoathirika zaidi ni pamoja na barabara ya Gusii, Pandit Nehru na Kenyatta ambapo idadi ya makahaba ni baina ya 80-100 kila usiku kwa wastani. Wakati mwingine, wao huendelea kumiminika hadi wakafikia 300 au zaidi.

Pia makahaba wamedhibiti barabara ya Kanu Street viungani mwa mji wa Nakuru, bila kusahau eneo la Pipeline, Kikopey na Salgaa kwenye barabara ya Nakuru-Eldoret.