Habari Mseto

Maduka 86 ya dawa yafungwa, dawa za serikali zatwaliwa

April 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA SHABAN MAKOKHA

MADUKA 86 ya kuuza dawa eneo la Magharibi yalifungwa na dawa za thamani ya mamilioni ya fedha kutwaliwa, kufuatia oparesheni kali iliyoendeshwa na Bodi ya Kudhibiti Dawa na Sumu(PDP) kuanzia Jumatatu.

Miongoni mwa dawa zilizotwaliwa ni za kutoka hospitali za serikali.

Maduka 20 yalikuwa katika Kaunti ya Kakamega, 10 kwenye kaunti ya Bungoma, mengine saba yalipatikana Vihiga huku mawili yakifungwa Busia.

Afisa aliyesimamia oparesheni hiyo Dkt Domnic Kariuki alifichua kwamba walinasa dawa za serikali zinazouziwa wananchi katika maduka hayo ya kibinafsi.

“Dawa za serikali zilipatikana kwenye maduka matatu ya kibinafsi katika Kaunti ya Kakamega. Wahudumu wa maduka hayo pia walikamatwa,” akasema Bw Kariuki.

Baadhi ya waliokamatwa walikuwa wahudumu wa maduka maarufu ya Amanda, Murhanda, Lugosh katikati mwa mji wa Kakamega na walifikishwa katika Mahakama ya Kakamega walikokabiliwa na mashtaka ya kupatikana na mali ya serikali.

Bw Kariuki pia alishangaa jinsi maduka hayo yenye leseni halali yalikuwa yakiendeshwa na watu wasiona ujuzi wowote kuhusu masuala ya kimatibabu.

“Tumewaagiza wataalam wa matibabu ambao wamehusishwa na biashara hii wafike mbele yetu ili wachukuliwe hatua kali za kinidhamu,” aklisema Bw Kariuki wakati wa kikao na wanahabari katika hoteli ya Golf, Kakamega.