• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Maraga aagiza korti zisaidie waraibu, zisiwatupe jela

Maraga aagiza korti zisaidie waraibu, zisiwatupe jela

NA KALUME KAZUNGU

JAJI Mkuu David Maraga, ameamuru mahakama za Lamu kuwatambua waathiriwa wa dawa za kulevya wanaofikishwa mbele ya mahakama, kama wagonjwa wanaohitaji msaada badala ya kuwachukulia kuwa wahalifu.

Katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa kituo cha kurekebisha tabia waathiriwa wa mihadarati eneo la Lamu mwishoni mwa juma, Bw Maraga aliwataka majaji na mahakimu wa mahakama hizo kuwatuma waathiriwa wa dawa za kulevya kwenye vituo vya kuwarekebisha tabia badala ya kuwapeleka gerezani.

“Nafurahi leo kwamba niko hapa kufungua rasmi kituo cha urekebishaji tabia kwa waathiriwa wa dawa za kulevya. Kwa wakati huu idara ya mahakama pia imekuwa ikitilia mkazo watumiaji wa mihadarati kusaidiwa ili kujitoa kwa maisha hayo,” alisema.

“Hii ndiyo sababu ninawataka majaji na mahakimu wa hapa Lamu ambalo ni eneo mojawapo lililoathirika na dawa za kulevya kubadili mbinu ya jinsi kesi za watumiaji wa dawa za kulevya zinavyoshughulikiwa. Tukiwa na kituo kama hiki hapa Lamu, kuna haja ya nyinyi majaji kuhakikisha waathiriwa wa matumizi ya dawa za kulevya wanaletwa hapa badala ya kuwasukuma gerezani,” aliongeza.

Alisema waathiriwa wa dawa za kulevya si wahalifu bali ni wagonjwa wanaohitaji msaada ili wapone.

Jaji Mkuu alisema mahakama itawaadhibu wasambazaji na wauzaji wa mihadarati kote nchini.

Aliitaka jamii ya Lamu kushirikiana na idara za usalama kwa kutoa ripoti kuhusu wasambazaji na wauzaji wa mihadarati ili wakamatwe na kushtakiwa.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Kukabiliana na Mihadarati nchini (NACADA), zaidi ya Wakenya 5 milioni wanajihusisha na dawa za kulevya.

Bw Maraga alitaja dawa za kulevya kuwa donda sugu sio kwa Lamu pekee bali nchi nzima.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma nchini (DPP), Noordin Haji, alisema ofisi yake tayari imeanza mazungumzo na ile ya Mkurugenzi wa Kesi za Jinai (DCI) na Inspekta Mkuu wa Polisi nchini (IG) ili kuona kwamba mbinu zinazotumika kuwasilisha kesi za makosa madogo madogo, ikiwemo za watumiaji wa dawa za kulevya, wanoiba kuku na mbuzi zinashughulikiwa.

You can share this post!

Maduka 86 ya dawa yafungwa, dawa za serikali zatwaliwa

Kaunti za Pwani zatahadharisha wakazi kuhusu mafuriko yajayo

adminleo