Pombe kwa wenye njaa yazua ghadhabu
NA ERIC MATARA
VIONGOZI wa kisiasa, watetezi wa haki za binadamu na maafisa wa afya sasa wanataka vyakula vya misaada vinavyotolewa kwa walio na njaa, vikaguliwe kabla ya kuwasilishwa kwa wakazi.
Mwenyekiti wa kundi la kutetea haki za binadamu la Peoples Power Watch, Bw James Karanja, aliwataka wasamaria wema wakome kupeleka vyakula alivyosema vinaharibu maadili ya wakazi wa Baringo.
Hii ni baada ya kampuni ya kimataifa ya madini ya Chuanshan kutoka Uchina kutoa msaada wa pombe na vyakula kwa wakazi wiki jana.
“Kama nchi tunafaa kuhakikisha vyakula vya misaada vinavyotolewa kwa watu wanaokabiliwa na njaa vinakaguliwwa na kuidhinishwa na maafisa wa afya. Hili lisipofanyika, huenda tukawapa watu vyakula hatari,” akasema Bw Karanja.
“Inasikitisha kwamba baadhi ya wasamaria wema wanatumia suala la njaa kuwadhihaki Wakenya. Naomba idara mbalimbali za serikali kuhakikisha chakula chote cha msaada ni salama kwa afya ya wananchi,” akaongeza.
Katika mahojiano na Taifa Leo, Mkurugenzi wa Afya ya Umma, Dkt Kepha Ombacho alishtumu kampuni ya Chuanshan kwa kutoa pombe kwa wakazi wa Baringo akisema kileo hicho ni hatari kwa watu walio na njaa
“Kitendo cha kampuni hiyo ya Uchina hakikubaliwi kamwe. Unawezaje ukawapa wenye njaa pombe? Msaada wowote wa vyakula unafaa kuhitimu viwango vya chakula cha binadamu kabla ya kusambazwa,” akasema Dkt Ombacho.
Wakati huo huo, viongozi kutoka Kusini mwa Bonde la Ufa wanataka kampuni hiyo kuchunguzwa kwa kuwapa wakazi pombe.
Mwenyekiti wa Jubilee katika Kaunti ya Nakuru, Peter Cheruiyot na wanachama wa Bunge la Kaunti ya Nakuru wakiongozwa na Peter Mbae, wametaka asasi za kisheria kufanya uchunguzi wa kina ili kujua sababu za kampuni hiyo kuwapa wakazi pombe.
Mbunge wa Lugari, Ayub Savula naye ameomba uchunguzi ufanywe dhidi ya Mbunge wa Tiaty, William Kamket ambaye alihudhuria hafla hiyo ya wiki jana.