Habari Mseto

Oparanya alalama kiwango cha elimu nchini kinadorora

April 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA SHABAN MAKOKHA

GAVANA wa Kaunti ya Kakamega, Wycliffe Oparanya, amesikita kwamba kiwango cha elimu nchini kinaendelea kushuka, baada ya serikali kutekeleza sera ya wanafunzi wote wa shule za msingi kujiunga na kidato cha kwanza.

Bw Oparanya alisema shule nyingi nchini zinaendelea kukosa miundomsingi bora kwa kuwa ufadhili wa masomo unaotolewa na serikali hautoshi kugharamia mahitaji yote.

“Shule katika kaunti kadhaa zinakosa madarasa ya kutosha na yaliyoko yako katika hali mbaya tena bila vifaa vya kutosha vya masomo. Katika shule nyingi, hitaji la kimataifa la mwalimu moja kuwafundisha wanafunzi 45 haliwezi kutimia kutokana na wingi wa wanafunzi. Pesa zinazotolewa na serikali pia hugharamia karo ya shule pekee,” alisema.

“Hata shule za kitaifa zimesalia kuwa jina tu kwasababu hazina miundombinu ya kuziwezesha kufikia hadhi yao. Tangu zikwezwe ngazi hadi kuwa za kitaifa, hakuna majengo au ukarabati wowote ulioendeshwa katika shule hizo,’’ akasema Bw Oparanya.

Akizungumza wikendi iliyopita katika Shule ya Upili ya Emabole, Bw Oparanya aliitaka serikali kuu kushauriana na zile za kaunti kabla ya kutekeleza baadhi ya sera mpya akisema sera hizo huathiri misaada ya ufadhili inayotolewa na kaunti.

“Wakati nilipokuwa Waziri wa Mipango nilianzisha mpango uliohakikisha shule mbili zilijengwa katika kila eneobunge na kukweza hadhi kama vituo vikuu vya kiakademia. Vile vile, nilihakikisha walimu 10,500 wa shule za msingi na wengine 2,100 wa shule za upili waliajiriwa kwa kandarasi ili kuhimili idadi kubwa ya wanafunzi waliokuwa wakijiunga na shule,” akaongeza Bw Oparanya.

Akaongeza, “Iwapo serikali kuu itahusisha magavana katika uundaji wa sera mpya, tungekuwa tukiendeleza ujenzi wa mabweni, madarasa, kumbi za shule, ofisi na makazi ya walimu.”

Alitaja msongamano unaoshuhudiwa katika baadhi ya shule kama sababu zinazodororesha viwango vya elimu.