Raila alijaribu kuniingiza 'box' mara 4 lakini nikakataa – Ruto
Na CHARLES WASONGA
NAIBU Rais William Ruto Jumanne usiku alifichua kuwa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga alimfikia mara kadha kwa mazungumzo kati yake na Jubilee kabla ya muafaka kati yake na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 9, 2018.
Kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen, Naibu Rais alisema Bw Odinga alijaribu kuongea naye mara nne lakini akadinda.
“Hebu nikupe historia kidogo. Kabla ya Raila Odinag kuanza mazungumzo na Rais kuhusu masuala ya handisheki alinifikia kwa mazungumzo. Alinifikia mara nne baada ya uchaguzi ili tufanye mazungumzo lakini nikakataa.
“Nilikataa kwa sababu mbili, kwanza katika Jubilee tuko na uongozi mkuu ambao ni Rais Kenyatta aliye pia kiongozi wa chama. Mazungumzo yoyote haswa kuhusiana na masuala ya kisiasa sharti yaanze naye.
“Sababu ya pili ni kwamba sikushawishiwa kwamba Raila alikuwa na nia njema kutaka mazungumzo nasi,” Dkt Ruto akafichua.
Alisema kuwa alikataa kutokana na historia mbaya ya Bw Odinga ya kuvunja vyama, kama alivyofanya alipoingia Kanu mnamo 1998.
“Alipoingia KANU aliibomoa na kuondoka na nusu ya mawaziri. Baadaye alipoungana na Kibaki mnamo 2003 chini ya Narc, serikali hiyo haikudumu kwa miaka miwili kabla ya kusambaratika. Hali hiyo ilimfanya Kibaki kutafuta usaidizi kutoka vyama vingine,” Dkt Ruto akasema.
Naibu Rais aliongeza kuwa katika kila jaribio la Bw Odinga la kutaka kuzungumza naye, yeye (Ruto) alimwarifu Rais kwamba hakuwa tayari kushiriki mazungumzo hayo.
Dkt Ruto aliendelea kufichua kwamba kando na kutuma wajumbe, Bw Odinga alimpigia simu mara mbili jambo ambalo lilimshtua.
“Mara mbili tuliongea kwa simu ningeelewa akisema… oh rais amekuchezea kwa kukupa mawaziri sita. Lakini nikamweleza kuwa mbeleni tulikuwa tukiendesha serikali lakini leo tuko na chama kimoja na rais ndiye kiongozi wa chama hiki,” akaeleza.
Dkt Ruto aliongeza kuwa kulingana na tathmini yake, Bw Odinga alikuwa akimaanisha kuwa yeye (Naibu Rais) hakutendewa haki na Rais katika uteuzi wa mawaziri hao sita.
Katika mazungumzo hayo yaliyoendeshwa na mtangazaji Hussein Mohamed, Ruto aliendelea kusema kuwa Rais Kenyatta alisaka maoni yake kabla ya kufanya mazungumzo na Bw Odinga.
“Rais Kenyatta alinijulisha kuhusu mpango wake wa kuzungumza na Bw Odinga na nikamweleza fikra zangu,” akasema bila kufafanua ikiwa fikra hizo zilizokuwa za kupinga au kuunga mkono muafaka huo.