Habari Mseto

KQ haina uwezo kutwaa usimamizi wa JKIA, bunge laambiwa

April 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MAMLAKA ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege Nchini (KAA) imepinga mpango unaoendelea wa kuiwezesha Shirika la Ndege Nchini (KQ) kutwaa usimamizi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kipindi cha miaka 30.

Jumatano usimamizi wa KAA uliambia Kamati ya Bunge kuhusu Uchukuzi, Ujenzi na Nyumba kwamba KQ haina uwezo wa kifedha na kiufundi wa kuendesha uwanja huo wa ndege.

Ikitoa mawasilisho yake kwa kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing, usimamizi wa KAA ulibainisha tofauti iliyoko baina ya uendeshaji shughuli za shirika la ndege na uwanja wa ndege huku ukielezea tashwishi yake kuhusu kufanikiwa kwa mpango huo.

Mpango huo unapangwa kutekelezwa chini ya mfumo wa unaoendeshwa na sekta ya kibinafsi – Privately Initiated Investment Proposal (PIIP).

Kupitia Afisa Mkuu Mtendaji Johnny Anderson na Mwenyekiti Issac Awuondo, KAA ilisema wazi kuwa KQ haina uwezo wa kifedha wa kuendesha shughuli za JKIA.

Wawili hao waliwaambia wabunge kwamba ipo haja kwa njia mbadala kutafutwa ya kuisaidia shirika la KQ kukabiliana na changamoto zinazoizonga.

Kwa mfano Mbw Anderson na Awuondo waliamba wabunge kwamba KQ inazongwa na mzigo wa madeni wa kima cha Sh5.4 bilioni kufikia Machi 31, mwaka huu.

“Tumewawekea presha tukiwataka watulipe deni lakini ukweli ni kwamba hawajaweza kulipa. Kama ingekuwa ni mashirika mengine ya ndege tungevuruga shughuli zao,” akasema Alex Gitari, ambaye ni Meneja wa Fedha katika KAA.

Alisema suala ya madeni sharti litiliwe maana katika mpango huo wa PIIP.

Bw Gitari aliiambia kamati hiyo kwamba KQ imeshindwa kulipa madeni yake licha ya kuweka mikataba mbalimbali.

“Baada ya kuchunguza mpango huo, tulibaini udhaifu mkubwa. Ikiwa mpango huo utaendelea, basi itatulazimu kulazimu kwamba maswali na masuala tulioibua yashughulikiwe kwanza,” Bw Anderson akasema.

“Sisi ni wasimamizi wa mali ya umma kwa hivyo sharti tushughulikie masuala yaliyoko kabla ya kuweka sahihi stakabadhi ya makubaliano.

Bw Anderson pia alielezea hofu kwamba ikiwa KQ itatwaa usimamizi wa KAA, usimamizi wa viwanja vingine 18 vya ndege vilivyoko nchini na vinavyosimamiwa na mamlaka hiyo utaathirika.

Alisema JKIA huchangia asilimia 80 ya jumla ya mapato ya KAA, ambayo ni Sh12 bilioni kila mwaka. Mapato hayo yanatumika kufadhili uendeshaji shughuli na utunzaji wa viwanja mbalimbali vya ndege nchini.

Wabunge waliibua suala la mgongano wa kimaslahi kwa upande wa Bw Awuondo ambaye kando na kuwa mwenyekiti wa KAA yeye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Benki ya Commecial Bank of Africa. Benki hii ni mojawapo ambazo inadai KQ mabilioni ya fedha kando na kumiliki hisa katika Shirika hilo la Ndege.

Baada ya kuwekewa presha nyingi, Bw Awuondo aliambia kamati hiyo kwamba yuko tayari kujiuzulu kutokana na hali hiyo.

Benki ya Commercial Bank of Africa (CBA) inamilikiwa na familia ya Rais Uhuru Kenyatta.

KQ inadaiwa Sh3.1 bilion na benki ya CBA, Sh2.1 bilioni (Benki ya NIC), Sh5.2 bilioni (Benki ya Equity), Sh3.5 bilioni (National Bank), Sh3.3 bilioni (Cooperative Bank), Sh2.1 bilioni (Benki ya DTB) na Sh2.1 bilioni (KCB).

Benki za CBA na NIC zinapanga kuungana, katika mpango ambayo unaendelea kukamilika.