HabariSiasa

Twanga pepeta ya Ruto na Raila

April 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

CHAMA cha ODM Jumatano kilikanusha vikali madai ya Naibu Rais, William Ruto kuwa Bw Raila Odinga alituma wajumbe kwake mara nne kumshawishi washirikiane kisiasa kabla ya handisheki mwaka 2018.

Taarifa hiyo ya ODM ilitaja kama uongo mtupu madai ya Dkt Ruto, na kusema kamwe Bw Odinga hawezi kushirikiana na Naibu Rais kisiasa katika hali yoyote ile.

Badala yake, ODM ilidai Dkt Ruto ndiye aliyetuma wajumbe wake kwa Bw Odinga akitaka washirikiane “kummaliza Rais Uhuru Kenyatta na watu wake”.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna alisema Dkt Ruto kwanza alimtuma Mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi kupitisha ujumbe kwa Bw Odinga kupitia kwa mfanyikazi mmoja katika ofisi ya Capitol Hill.

“Ujumbe wa Ruto kwa Bw Odinga ulisema ndiye aliyekuwa akishikilia usukani wa kuendesha taifa, na angetaka kufanya kazi na Bw Odinga. Lakini Bw Odinga alimwagiza mfanyikazi huyo kukomesha mawasiliano na Sudi baada ya kufahamu lengo la Ruto lilikuwa gani,” akadai Bw Sifuna kwenye ujumbe wake uliojaa ukali.

Bw Sifuna alisema kuwa Dkt Ruto hakufa moyo na badala ya kukoma alimtuma waziri wa zamani mwanamke kutoka Rift Valley, akipendekeza kuwa Bw Odinga ashikane naye ili “wasaidiane kuthibiti Uhuru na watu wake”.

“Waziri huyo wa zamani alijaribu mara nne kumshawishi Bw Odinga, ambaye alikataa pendekezo la Ruto,” akasema Bw Sifuna.

Akaendelea: “Alijaribu kumshawishi Bw Odinga kwa ujumbe kuwa washirikiane ‘kumaliza adui yetu sote’, lakini kinara wa ODM alikataa.”

Kwenye mahojiano na Citizen TV mnamo Jumanne usiku, Dkt Ruto alidai kwamba Bw Odinga alimpigia simu na hata kumtumia wajumbe akitaka washirikiane kisiasa lakini akakataa.

“Raila alinisihi mara nne akitaka tuzungumze lakini nikakataa. Nilimwambia kwamba Jubilee tuna kiongozi mmoja tu,” akasema Dkt Ruto.

Naibu Rais alisema kuwa alimkwepa Bw Odinga kwa sababu aliamini kwamba alikuwa na ‘nia fiche’.

“Tulizungumza na Raila kwa simu baada ya Rais Kenyatta kuteua mawaziri sita wa kwanza. Bw Odinga aliniambia kwamba nilipigwa chenga katika uteuzi huo lakini mimi nikakataa kuzungumza naye. Nilimwambia kwamba rais ndiye mkuu wa chama na hatukuwa ndani ya serikali ya muungano.”

Dkt Ruto alisisitiza kwamba anaunga mkono handisheki kwani imeleta manufaa, licha ya ODM kumtaja kama adui mkuu wa mwafaka huo.

“Handisheki imesaidia kwani hakuna maandamano, watu hawazozani mitaani na biashara zinaendeshwa kwa utulivu,” akasema Dkt Ruto.

Alisema atakabiliana na Bw Odinga endapo atajaribu kusambaratisha Jubilee.

Dkt Ruto alisema wanasiasa wa Jubilee wanaompinga kuwania urais 2022 ni wanachama wa zamani wa ODM, na watu waliokataliwa na wapigakura katika uchaguzi uliopita.

Dkt Ruto pia alikariri kuwa hakufadhili mwaniaji yeyote katika chaguzi ndogo za Ugenya na Embakasi Kusini, ambapo chama cha ODM kilipoteza.