Shujaa yakutanishwa na wakali Fiji na Samoa London Sevens
Na GEOFFREY ANENE
DROO ya duru ya tisa ya Raga ya Dunia itakayofanyika jijini London nchini Uingereza mnamo Mei 25-26, 2019, imetangazwa, huku Kenya ikitiwa Kundi B pamoja na Fiji, Samoa na Ufaransa.
Shirikisho la Raga Duniani World Rugby limefanya droo hiyo baada ya duru ya nane kukamilika nchini Singapore mnamo Aprili 14.
Limekutanisha Afrika Kusini, Argentina, Canada na Japan katika Kundi A, Uingereza, New Zealand, Scotland na timu alikwa katika Kundi C nazo Marekani, Australia, Wales na Uhispania zinaunda Kundi D.
Kenya, Wales na Japan zinashikilia nafasi tatu za mwisho kwenye Raga ya Dunia ya msimu huu wa 2018-2019 zikikaribiana sana kwa alama baada ya kuzoa alama 26, 25 na 22 mtawalia katika duru nane za kwanza.
Timu hizi tatu ziko katika vita vikali vya kuepuka kumaliza msimu katika nafasi ya 15, ambayo atakayeishikilia baada ya duru ya mwisho nchini Ufaransa mnamo Juni 1-2 ataondolewa kwenye ligi hii ya kifahari.
Shujaa ya Kenya, ambayo msimu uliopita wa 2017-2018 ilijiandikia historia ya kuzoa zaidi ya alama 100, ilipata 104, itakuwa na kibarua kigumu katika kundi lake hasa kutokana na kwamba ina rekodi mbaya sana dhidi ya Fiji, Samoa na Ufaransa.
JEDWALI LA SINGAPORE SEVENS
Taifa Alama
Afrika Kusini 22
Fiji 19
Uingereza 17
Marekani 15
Samoa 13
New Zealand 12
Argentina 10
Australia 10
Ufaransa 8
Scotland 7
Canada 5
Wales 5
Kenya 3
Uhispania 2
Hong Kong 1
Japan 1
MSIMAMO WA RAGA YA DUNIA 2018-2019:
Taifa alama
Marekani 145
Fiji 142
New Zealand 130
Afrika Kusini 121
Uingereza 107
Samoa 87
Australia 80
Argentina 79
Ufaransa 71
Scotland 62
Uhispania 47
Canada 41
Kenya 26
Wales 25
Japan 22