Habari MsetoSiasa

'Tangatanga' wataka wapinzani watimuliwe Jubilee

April 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NDUNG’U GACHANE na KENNEDY KIMANTHI

MIGAWANYIKO ya kisiasa jana ilizidi kutokota katika Chama cha Jubilee (JP), baada ya kundi moja la wabunge kushinikiza kufurushwa kwa wenzao ambao wanampinga Naibu Rais William Ruto.

Kundi hilo, maarufu kama ‘Team Tanga Tanga’ linakitaka chama hicho kuitisha mkutano wa haraka wa wabunge wote ili kuwaondoa wenzao wa kundi la ‘Kieleweke’ wanalodai linaunga mkono muungano wa Upinzani (NASA).

Wale waliozungumza na Taifa Leo, walisema wataendelea kuushinikiza uongozi wa chama kuhakikisha kuwa kundi la ‘Kieleweke’, limechukuliwa hatua kwa kutomheshimu Dkt Ruto.

Kundi linadai kuwa wanachama wa ‘Kieleweke’ wamekuwa wakitoa kauli za kumkosea heshima, licha ya kuwa mojawapo wa viongozi wakuu wa chama.

Kundi la ‘Kieleweke’ linawajumuisha Mbunge Maalum Maina Kamanda, aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa JP, Bw David Murathe, wabunge Maoka Maore (Igembe Kaskazini), Muturi Kigano (Kangema) na Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), ambaye ndiye mwanzilishi.

Lakini Jumapili, Katibu Mkuu wa JP, Bw Raphael Tuju alipuuzilia mbali pendekezo hilo, akisema kuwa lazima taratibu za chama zizingatiwe katika kumwondoa mwanachama yeyote.

Vile vile, alipuuza uwepo wa makundi hayo mawili, akisema kuwa hayana misingi yoyote ya kisiasa.

“Hakuna kundi lolote ambalo limetangaza kuwa si mwanachama wa Jubilee ama kuanza uhusiano na makundi mengine ya kisiasa,” akasema Bw Tuju.

Kulingana na kipengele 14 (7) cha Sheria ya Vyama vya Kisiasa, mwanachama wa chama chochote anaweza kuondolewa tu ikiwa amekiuka katiba ya chama husika.

Vile vile, lazima mwanachama apewe nafasi ya kutosha kujitetea kulingana na taratibu zilizowekwa katika katiba hiyo.

Baadhi ya sababu ambazo zimekuwa zikizua migawanyiko katika chama hicho ni ushindani wa urithi wa Rais Uhuru Kenyatta, muafaka wa kisiasa kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga na siasa za uchaguzi mkuu wa 2022.

Jumapili, mbunge wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro, alidai kuwa kundi la ‘Kieleweke’ “linamfanyia kazi Bw Odinga na muungano wa NASA kuisambaratisha Jubilee.”

“Wanachama wengi wa kundi hilo walikuwa washauri na wanachama wa ODM. Tumekuwa wazi kuwa lengo kuu la muungano wa NASA lilikuwa kutumia handisheki ili kuleta migawanyiko Jubilee. Wanalenga kuzua migawanyiko kama walivyofanya baada ya chama cha Kanu kuungana na LDP,” akasema Bw Nyoro kwenye mahojiano.

Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Kirinyaga, Bi Wangui Ngirichi naye alisema kuwa ni kinyume na kanuni za Jubilee kwa mwanachama wake kuunga mkono chama ama kundi lingine la kisiasa.

“Hata ODM walimfurusha mbunge wa Malindi , Aisha Jumwa kwa dai la kuunga mkono Jubilee. Baadhi ya viongozi hawakuchaguliwa na wananchi, lakini wamekuwa wakiupigia debe Upinzani, kiasi cha kushinikiza muungano kati ya Jubilee na ODM. Ni lazima waondolewe katika Jubilee ili wapate muda wa kutosha kumfanyia kampeni Odinga,” akasema.

Hata hivyo, Bw Wambugu alisema kuwa ‘Kieleweke’ haimfanyii kampeni kiongozi yeyote.