• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Dereva kikaangoni kuhusu madaktari wa Cuba

Dereva kikaangoni kuhusu madaktari wa Cuba

Na RICHARD MUNGUTI

DEREVA aliyekuwa anawaendesha madaktari wawili wa Cuba waliotekwa nyara katika kaunti ya Mandera Ijumaa na magaidi alifikishwa katika mahakama ya Milimani Nairobi na kuamriwa azuiliwe rumande kwa muda wa siku 15.

Bw Isaac Ibrein Elbow alifikishwa mbele ya hakimu mkazi Bi Muthoni Nzibe na maafisa wa kupambana na ugaidi (ATPU) walioomba azuiliwe katika afisi zao kwa siku 15 kuhojiwa.

Bi Nzibe alielezwa Madaktari hao walitekwa nyara na watu wanaoshukiwa kuwa magaidi wa Al Shabaab mjini Mandera wakielekea kazini.

Walikuwa wanatoka katika makazi yao kuelekea hospitali ya Mandera Level 5 walipokuwa wanahudumu.

Madaktari hao Dkt Assel Corera na Dkt Landyz Rodrigues walivamiwa na magaidi waliokuwa ndani ya magari aina ya Probox na kumwua mlinzi wao kabla ya kutoroka na wawili hao.

Hakimu Nzibe alielezwa kuwa Madaktari hao waliokuwa wanatoa huduma kwa wananchi wa Kenya na mataifa jirani walipelekwa Somalia.

Bw Elbow alitiwa nguvuni mjini Mandera punde tu baada ya kisa hicho cha utekaji nyara na kusafirishwa hadi Nairobi kuhojiwa. Mahakama ilielezwa kuwa uchunguzi unaendelea.

“Uchunguzi katika kesi hii unaendelea. Maafisa wa ATPU wakishirikiana na maafisa wa uchunguzi wa kimataifa wanaendelea na uchunguzi kubaini waliko Madaktari hao wawili,” hakimu alielezwa.

Mahakama ilifahamishwa kuwa Bw Elbow atahojiwa ibainike ikiwa alihusika ama kushiriki katika kisa hicho cha utekaji nyara.

Naomba mshukiwa huyu azuiliwe kwa muda wa siku 15 kuwasaidia polisi katika uchunguzi wao,” hakimu alifahamishwa.

Akitoa uamuzi hakimu alisema polisi wanahitaji kupewa muda kukamilisha uchunguzi huo aliosema utasambaa hadi taifa jirani. Mahakama iliamuru kesi hiyo itajwe Mei 29, 2019.

Vikosi vya usalama vya Kenya vilijitosa katika harakati za kuwasaka magaidi hao wa Al Shabaab waliotoroka na madaktari hao.

Ndege za kijeshi zilionekana katika miji ya Mandera nchini Kenya na kusafiri hadi mji wa Bulahawa nchini Somalia.

Habari za kijasusi zilidokeza kuwa madaktari hao wanazuiliwa katika eneo la El Adde jimbo la Gedow nchini Somalia.

Polisi nchini Kenya wanafanya uchunguzi wa kina kuwatia nguvuni wahusika, Bi Nzibe alielezwa.

You can share this post!

Korti yawaachilia wanakamari 13 wakasajiliwe Huduma Namba

Majaji 14 motoni akiwamo David Maraga

adminleo