Jeshi latangaza mageuzi mapya Sudan japo presha ya raia ingalipo

Na MASHIRIKA

BARAZA tawala la kijeshi nchini Sudan limetangaza harakati mpya za mageuzi yanayolenga kuwaridhisha waandamanaji ambao wamekuwa wakishinikiza kuanzishwa kwa utawala wa kiraia.

Haya yanajiri baada ya kuondolewa mamkakani kwa aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu wa taifa hilo, Omar al-Bashir.

Miongoni mwa mageuzi hayo, ni kubadilishwa kwa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NISS) ambalo limelaumiwa pakubwa kwa kuwakamata na kuwazuilia waandamanaji bila hatia yoyote.

Msemaji wa utawala huo Shams Kabashi alisema kuwa baraza hilo pia litawakamata viongozi wa serikali ambao walikuwa wakitumia mamlaka yao kuwahangaisha waandamanaji.

Kulingana naye, mojawapo ya matakwa makuu ya vyama vya kisiasa na makundi ambayo yalishiriki katika maandalizi ya maandamano hayo ni mageuzi ya NISS.

Shirika hilo pia linalaumiwa kwa kuwaua na kuwajeruhi baadhi ya waandamanaji hao.

Alisema kuwa baraza hilo limemteua Luteni Jenerali Abu Bakr Mustafa kuwa kiongozi wake baada ya kujiuzulu kwa Salah Abdallah.

Vilevile, alitangaza kuondolewa kwa Jenerali Awad Ibn Auf kutoka nafasi yake kama Waziri wa Ulinzi.

Jenerali huyo alikuwa amechukua mamlaka, akisema kuwa ataliongoza taifa hilo kwa miaka miwili katika serikali ya mpito, lakini akalazimika kijuzulu kutokana na shinikizo za waandamanaji.

Nafasi hiyo ilichukuliwa na Luteni Jenerali Fattah al-Burhan aliyeapa “kuukabili vikali” utawala wa Bashir.

Mazungumzo

Alisema atawaachilia wafungwa wote wa kisiasa na kufanya mazungumzo na makundi yaliyoshiriki katika maandamano hayo.

Saa chache baada ya mabadiliko hayo, kundi la wajumbe kumi wanaowakilisha waandamaji lilisema kuwa litaridhishwa na mageuzi hayo tu ikiwa wanajeshi watampa mamlaka kiongozi wa kiraia.

Mnamo Jumapili, Kundi la Wataalamu la Sudan (SPA) ambalo liliongoza maandamano hayo lilisema kuwa litaendeleza shinikizo zake hadi pale kiongozi wa kiraia atapewa mamlaka.

Kwenye matakwa tisa ambayo liliwasilisha kwa utawala huo, SPA inataka akaunti zote za maafisa wakuu wa serikali ya Bashir kufungwa, kufutwa kazi kwa majaji wote na viongozi wa mashtaka, kukamatwa kwa Bashir na aliyekuwa mkuu wa NISS, Mohamed Atta.

Miongoni mwa maafisa wakuu ambao wamefutwa kazi kufikia sasa ni aliyekuwa balozi wa taifa hilo nchini Uswizi.

Jeshi pia limesema kuwa polisi wote waliokamatwa kwa kushiriki katika maandamano hayo pia wataachiliwa huru.

Baraza pia lilisema kuwa litabuni kamati ambayo itachukua mali ya chama cha Bashir.