Wafanyakazi wa Sony Sugar wagoma kudai malipo
Na ELIZABETH OJINA
WAFANYAKAZI zaidi ya 2,000 wa Kampuni ya Sukari ya Sony, Jumanne waligoma kulalamikia kutolipwa mishahara yao.
Waliandamana mjini Awendo, Kaunti ya Migori wakitaka kulipwa karibu Sh100 milioni kwa jumla.
Walisema waliamua kufanya mgomo kwa sababu wasimamizi wa kampuni hiyo walishindwa kutekeleza ahadi ya kulipa mishahara wanayodai kikamilifu.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mashamba Makubwa ya Miwa Kenya, Bw John Ogutu alisema hawajalipwa kwa miezi mitatu.
“Vibarua hawajapokea mishahara kwa miezi mitatu iliyopita na wafanyakazi walioajiriwa nafasi za kudumu hawajalipwa mishahara ya Februari na Machi,” akasema Bw Ogutu.
Walikuwa wamewasilisha ilani ya siku saba kabla kuanza mgomo, mnamo Machi 23.
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya SONY, Bw Bernard Otieno, alisema yuko likizoni na hangeweza kuzungumzia suala hilo.
Kwa upande mwingine, afisa wa uhusiano mwema katika kampuni hiyo, Bi Ruth Opole alisema walikuwa mkutanoni kujadiliana jinsi ya kutatua tatizo hilo na angetoa taarifa baadaye.
Wawakilishi wa wafanyakazi walisisitiza hawatarudi kazini hadi mishahara yao ilipwe.