• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Meneja wa Kenya Power asukumwa kwa kona

Meneja wa Kenya Power asukumwa kwa kona

Na RICHARD MUNGUTI

MENEJA wa mauzo katika kampuni ya umeme ya Kenya Power (KP) Jumanne alifichua aliongeza kampuni nne ambazo hazikuorodheshwa na Kamati ya Ukaguzi Juni 2017.

Bw Bernard Ngugi aliyekuwa akitoa ushahidi katika kesi ambapo meneja mkurugenzi wa KP Dkt Ken Tarus ameshtakiwa kwa kufanya njama za kuilaghai kampuni hiyo Sh159 milioni akishirikiana na wengine alisema sheria ilimuruhusu kufanyia marekebisho ripoti hiyo kabla ya kampuni zilizofaulu kujuzwa.

Bw Ngugi alimweleza hakimu mkuu wa mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Lawrence Mugambi kuwa aliongeza kampuni hizo baada ya kukagua kampuni 1,354 zilizowasilisha maombi ya kupewa kazi na KP.

Bw Ngugi aliyekuwa anahojiwa na mawakili Katwa Kigen, Dunstan Omari na Cliff Ombeya alisema kampuni zilizoidhinishwa na aliyekuwa mkurugenzi mkuu Dkt Ken Tarus zilifikia 529.

Awali kamati ya ukaguaji iliwajumuisha Wahandisi Daniel Tare, James Muriuki, James Njehia, Noah Omondi na Bernard Muturi ilikuwa imeteua makampuni 525 kati ya 1,354 yaliyokuwa yamewasilisha maombi.

Mawakili walimwuliza Ngugi sababu ya kurekebisha ripoti hiyo baada ya siku 45.

Alijibu alikuwa ameenda likizo ndefu na hakuwa ameona ripoti mdogo wake alikuwa ametayarisha.

“Nilitoa maoni yangu baada ya kurekebisha orodha iliyokuwa imepelekwa kwa Dkt Tarus kisha nikamwuliza aongeze majina ya kampuni hizo nne,” alijibu Ngugi.

Shahidi huyo alikanusha madai kuwa yeye ni miongoni mwa wale waliofanya njama za kuifilisi KP.

Kesi inaendelea kusikizwa Jumatano.

You can share this post!

Msitarajie mvua Aprili na Mei – Idara

Ndani kwa mashtaka ya kubambwa wakiwa na...

adminleo