TAHARIRI: Hifadhi ya chakula ingetusaidia sana
NA MHARIRI
Kutokana na tangazo la Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini kuwa hakutakuwa na mvua yoyote msimu huu, wengi waliotarajia mvua ya masika wamevunjika moyo kabisa. Idara hiyo yahusisha uhaba huo wa mvua na mabadiliko katika hali ya anga.
Sehemu nyingi nchini zimeshuhudia hali ya ukame msimu huu na Idara hiyo ilisema kuwa ni maeneo machache tu ambayo yalipokea mvua chache. Maeneo hayo ni Kisii, Nyamira, Bungoma, Trans-Nzoia, Kakamega, Busia, Homa Bay na Kericho.
Maeneo ya Kati kama Kiambu, Meru na Nairobi pia yalipokea mvua kiasi tu. Mapema mwaka huu, idara hiyo ilikuwa imetabiri kuwa mvua ya masika ingeanza kunyesha mwezi Aprili na si Machi kama ilivyo kawaida. Vilevile, ilikuwa imeonya kuhusu kupungua kwa mvua ambayo ingenyesha.
Hali hii bila shaka itasababisha si tu uhaba mkubwa wa maji bali pia chakula na hasa mahindi ambayo Wakenya wengi wanategemea kwa ajili ya maisha yao.
Kwa bahati mbaya, Wakenya hawajifunzi kutokana na majanga kama haya yaliyowahi kutokea awali.
Tunahitaji kuwa tulihifadhi chakula cha kutosha ili kukidhi hitaji la chakula kwa wakati kama huu.
Maeneo mengi nchini yameripotiwa kukumbwa na baa la njaa nchini na kumekuwa na juhudi za kimakudusi kuyafikishia msaada wa chakula, maji na hata matibabu.
Ukweli ni kwamba, uhaba wa mahindi ambao tayari umeripotiwa nchini utaumiza Wakenya wengi.
Mosi, gharama ya maisha itapanda kutokana na mfumko wa bei ya mafuta ambayo tayari imeongezwa. Baadhi ya wakulima wameelezea hofu yao kufuatia hatua ya ERC kuongeza bei ya mafuta.
Si ajabu bei ya mahindi sasa ikatimia Sh5,000 kwa sababu ya ukosefu wa bidhaa hiyo adhimu nchini.
La kustaajabisha ni kwamba hata baada ya wakulima kuiuzia Bodi ya Nafaka Nchini NCPB mamilioni ya magunia ya mahindi, eti sasa kuna uhaba wa mahindi. Si ajabu hiyo.
Waziri wa Ugatuzi anapaswa kujitokeza wazi na kuwaambia wananchi kimasomaso hali halisi kwa sasa. Wakenya wasitaabike kwa mipango duni ya serikali kuhusu uhifadhi wa chakula. Tunapaswa, kama taifa, kujifunza namna ya kuweka akiba ya chakula ili tusitaabike katika nyakati kama hizi.