• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
AKILIMALI: Aina ya sungura bora na walio rahisi zaidi kufuga nchini

AKILIMALI: Aina ya sungura bora na walio rahisi zaidi kufuga nchini

Na CHRIS ADUNGO

AKILIMALI ilipozuru Shule ya Upili ya Mercy Njeri katika mtaa wa Kiamunyi viungani mwa mji wa Nakuru, tulipata mengi ya kujifunza na kuiga kutoka kwa msomi anayefuga sungura kama uraibu tu.

Anawahimiza vijana wanaopania kujiendeleza kimaisha wasitegemee masomo peke yake bali wawe na njia mbadala za kujiongezea kipato hasa katika sekta ya kilimo, hususan ufugaji.

“Teknolojia ya kisasa imerahisisha hali ya maisha, upatikanaji wa maarifa, usambazaji wa elimu na mbinu mwafaka za kibunifu katika kukuza ndege na mifugo wa kila aina,” alieleza Bi Akai, mwalimu wa somo la Kilimo shuleni humo, Bi Mercy Njeri.

Sungura ni miongoni mwa wanyama wenye nyama iliyo na kiwango kikubwa cha protini.

Ni kiumbe aliye na kiwango kidogo cha mafuta katika nyama yake kinyume na wanyama wengine kama vile ng’ombe na mbuzi. Wanyama hawa huchukua muda mfupi sana kukomaa, takriban miezi minne au mitano.

Wakulima wanaoshughulikia ufugaji wa sungura wanaungama kwamba viumbe hawa huzaa kati ya watoto wawili hadi wanane ilmradi tu uwatimizie mahitaji yao ya kila siku kuanzia hewa safi, maji ya kutosha na chakula hasa majani yanayotokana na mimea kama vile sukumawiki, pamoja na mizizi ya shambani na mwituni inayoweza kupatikana katika vichaka.

Sungura huchukuwa muda mfupi sana kutungwa mimba na kupata vimwana (vitungule) ambao huzaliwa baada ya wiki nne; yaani mwezi mmoja.

Mwalimu Susan Akai anasema mradi huu wa ufugaji wa sungura ulianzishwa na mmoja wa wanafunzi wake kwa mtaji wa Sh1,000 naye akashika usukani kuupanua zaidi mnamo 2017 alipogundua kwamba manufaa yake hayana kifani.

Kwanza, palihitajika sehemu ndogo ya kusimamishia kibanda kidogo cha mbao na waya uliozunguka ili kuwalinda dhidi ya wanyama hatari au wezi, hasa ikizingatiwa kwamba ni wanyama wanaoweza kuchukulika upesi.

Zaidi ya kuwa kivutio kikubwa kwa wageni wanaozuru Shule ya Upili ya Mercy Njeri inayopatikana katika eneo la Kiamunyi, Nakuru, sungura pia ni fahari kwa wanafunzi wanaofanya utafiti hasa katika somo la Zaraa ambapo wanaweza kupata maarifa ya moja kwa moja kuhusu masuala ya ufugaji wa wanyama wadogo.

Sungura wamefanywa kuwa kitega uchumi kwa wakulima wanaowafuga kwa wingi ndani na nje ya mji wa Nakuru.

Spishi au aina ya sungura ambao huendana vyema na hali ya anga humu nchini ni California White na Flemish Giant lakini hii haimaanishi kwamba tujikite katika ufugaji wa sungura wa sampuli hiyo tu.

Tukumbuke kuwa Carlifonia White wanaweza kustahimili joto jingi na pia baridi kali kwa kiwango sawia. Tulipowatembelea, tuligundua kwamba sungura ni wanyama safi sana, na wanapokomaa, huwa ana uzani wa takriban kilo saba.

Cha msingi ni kwamba, mkulima anafaa kuwaepusha wanyama hawa dhidi ya baridi kali ambayo inaweza kuwasababishia maradhi ya ngozi, na ndiyo maana wafugaji wanahimizwa kutumia makuti, nyasi na mabaki ya mbao katika sehemu ambapo ni baridi kupita kiasi hasa nyanda za juu.

Chanjo

Sungura wanahitaji kupewa chanjo kila mara kwa wakati mwafaka ili kuwakinga dhidi ya ugonjwa wowote, na wala mkulima asiwape chakula kichafu.

Juhudi za kutafuta soko la sungura pamoja na bidhaa zake huwa rahisi sana kwani wengi wa sungura hufugwa na watu kama sehemu ya uraibu wao.

Wakati mwingine, sungura hufugwa kwa ajili ya kitoweo chake.

Mbali na haya, wao huuzwa kulingana na kilo ambapo kilo nne huuzwa kwa kima cha Sh400.

Nyama yake hulazimika kukaushwa kabla ya kuliwa kwani ina maji mengi sana yanayotokana na chakula chake chenye kiwango cha juu cha unyevu.

You can share this post!

Kaka zake Bashir nao wanyakwa Museveni akijitolea kumpa...

Wito kwa wazazi mitaani wapeleke wana kwa taasisi za ufundi

adminleo