Kuna njama fiche ya kuagiza mahindi ng’ambo – Keter
Na CHARLES WASONGA
MBUNGE wa Nandi Hills Alfred Keter amepinga madai ya baadhi ya wasagaji kwamba, kuna uhaba wa mahindi nchini akisema, hicho ni kisingizio cha wao kutaka serikali iwaruhusu kuagiza mahindi kutoka nje.
Akiongea na wanahabari Alhamisi katika majengo ya bunge, Bw Keter alisema wakulima bado wanahifadhi zaidi ya magunia 25 milioni ya mahindi katika stoo zao baada ya kukosa kuiuzia serikali kwa bei duni ya Sh2,500 kwa gunia moja la kilo 90.
Aliitaka serikali kununua mahindi kutokwa kwa wakulima hao kwa bei ya sasa ya Sh3,500 “badala ya kuitikia kauli za matapeli hawa ambao wanataka wafaidike kwa kuagiza mahindi kutoka nje”.
“Napinga kabisa kauli ya watu hawa. Kati ya magunia 44 milioni ambayo wakulima wetu kutoka maeneo ya North Rift na maeneo mengine ya nchini walivuna msimu uliopita bado wanahifadhi zaidi ya magunia 25 milioni. Serikali inunue mahindi haya kwa Sh3,500 badala ya kuruhusu uagizaji wa mahindi kutoka nje,” akasema Bw Keter.
Mbunge huyo alisema wengi wa wakulima hawakuuza mahindi yao kwa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) mapema mwaka huu, hali iliyopelekea bodi hiyo kupokea magunia 300,000 pekee badala ya magunia 2 milioni ambayo serikali ililenga kununua kwa bajeti ya Sh5 bilioni.
“Hii ina maana kuwa serikali bado inahitaji kununua magunia 1.7 milioni kutoka kwa wakulima ili kutosheleza hitaji lake la magunia 2 milioni. Hii ndio maana napendekeza serikali ijaze pengo hilo kwa kununua mahindi kutoka kwa wakulima kwa bei ya sasa,” Bw Keter akasisitiza.
Alisema wafanyabiashara walaghai na washirika wao ambao wamekuwa wakiwahimiza wakulima wa mahindi katika eneo la North Rift kuachana na uzalishaji wa mahindi na badala yake kukumbatia kilimo cha parachichi (avocado) ndio wanaoeneza uvumi kwamba kuna uhaba wa mahindi nchini ili waweze kufaidi kupitia uagizaji wa mahindi kutoka nje walivyofanya 2017.
Naibu Rais William Ruto amekuwa akiwashauri wakulima kukoma kutegemea kilimo cha mahindi pekee huku akiwataka kukumbatia kilimo cha matunda kama vile avocado yenye soko kubwa katika mataifa ya ng’ambo.
Kauli hiyo iliwakasirisha Bw Keter na wabunge Silas Tiren na Joshua Kuttuny waliodai kuwa hiyo ilikuwa sehemu ya mpango wa Dkt Ruto kufifisha kilimo cha mahindi nchini kuwezesha uagizaji mahindi kutoka nje.
Jana, Bw Keter alisema haikuwa sawa kwa serikali kuagiza mahindi kutoka nje kwa Sh3,900 kwa gunia moja la kilo 90 mnamo 2017 ilhali mwaka huu ikaamua kununua mahindi kutoka kwa wakulima kwa bei ya hasara ya Sh2,500.