• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Vita ndani ya ODM vilivyopunguza umaarufu wa ‘Baba’

Vita ndani ya ODM vilivyopunguza umaarufu wa ‘Baba’

NA CECIL ODONGO

IMEBAINIKA kwamba migogoro na ubabe kati ya viongozi ni baadhi ya masuala yanayoendelea kudidimiza umaarufu wa chama cha ODM hasa baada ya kupoteza kwenye chaguzi ndogo za maeneobunge ya Ugenya na Embakasi Kusini mapema mwezi huu.

Ingawa chama hicho kinachoongozwa na Kinara wa upinzani Raila Odinga kimekuwa dhabiti na hata kujivunia idadi kubwa ya wabunge miaka ya nyuma, duru zinaeleza kwamba kukosekana kwa njia maalum ya mawasiliano na washirika wa Bw Odinga kuzozana zinaelekea kupunguza umaarufu wake kabisa iwapo hatua madhubuti haitachukuliwa.

Seneta wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed, Katibu wa ODM Edwin Sifuna na Mwenyekiti John Mbadi ndio wanaohusika kwenye vita vya kudhibiti chama, kila moja akijinaki kuwa na uhusiano wa karibu na Bw Odinga.

Mgawanyiko wa wazi ulidhihirika wakati Bw Junet Mohamed ambaye ni Mkurugenzi wa uchaguzi wa ODM alipokosa kabisa kuhudhuria kampeni za kumpigia debe mgombeaji wao Chris Karan, duru zikiarifu haonani uso kwa macho na Bw Orengo aliyeongoza kampeni hizo.

“Chaguzi ndogo za Ugenya na Embakasi Kusini sasa zimepita. Tunawashukuru wafuasi wetu waliojitokeza na kupiga kura. Tunawashukuru kwa kuonyesha nidhamu ya hali ya juu na tunaheshimu uamuzi wa raia,” akasema Bw Mohamed baada ya Bw Karan na Irshad Sumra kushindwa na Mabw David Ochieng’ wa Movement for Democracy and Growth (MDG) na Musili Mawathe wa chama cha Wiper mtawalia.

Hata hivyo, Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati anahoji kwamba ODM inaporomoka kwa sababu viongozi wake wa sasa walipewa tu viti hivyo bila kuvitolea jasho baada ya kutibuka kwa uchaguzi ulioandaliwa katika uga wa MISC Kasarani mwaka wa 2014.

“Ni wakati wa ODM kujisuka upya kwa kuandaa uchaguzi ambapo maafisa wa chama watachaguliwa na wajumbe ili nyadhifa zinazoshikiliwa zitathaminiwe na washikilizi. Maafisa wa sasa wa ODM walipewa nafasi za kuongoza chama bila uchaguzi kuandaliwa na hilo limechangia tofauti zinazoshuhudiwa.

“Kwa sasa inaonekana vita vikali vimeanzisha na Mabw Mbadi na Mohamed ili kumsawiri Bw Orengo kama mtu asiyefaa kuwa karibu na Bw Odinga. Hii ni wazi kwa kuwa wamesisitiza mara kadhaa kwamba seneta huyo wa Siaya hawezi kuzungumza kwa niaba ya ODM kwa kuwa hashikili cheo chochote chamani,” akasema Bw Andati.

Kauli ya Bw Andati inaafiki kwa kuwa Bw Mbadi alijitokeza wazi na kupinga kauli tata ya Bw Orengo kuwa Rais Uhuru Kenyatta alikuwa amekubali kumuunga mkono Bw Odinga katika uchaguzi mkuu wa 2022 baada ya wawili hao kuamua kushirikiana.

“Chama cha ODM kinaendea mamlaka ya kisiasa na tunaandaa mikutano hii macho yetu yakielekezwa 2022. Ushindani mkali wa kupata mamlaka utatokana na ushirikiano mkubwa wa ODM na Jubilee ambapo Rais Uhuru Kenyatta atakuwa na majukumu makubwa ya kutekeleza,” akasema Bw Orengo akihojiwa na kituo kimoja cha habari nchini.

Ni matamshi hayo yaliyomkoroga nyongo Bw Mbadi na akajitokeza kumshtumu Bw Orengo akisema alikuwa akiwasilisha maoni yake kibinafsi wala si msimamo wa chama.

“Chama cha ODM hakijaingia kwenye mkataba wa kisiasa na chama kingine au mtu yeyote. Chama kina njia na kanuni za kuripoti kuhusu masuala hayo wala kinara wetu hajatueleza kuhusu makubaliano au muungano wowote.

“Handsheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga ina ajenda 9 na haimaanishi kwamba tumeingia kwenye mkataba wa kisiasa tukilenga 2022, tukishirikiana na Rais,” akasema Bw Mbadi akimjibu Bw Orengo.

Hata hivyo, Bw Andati anathibitisha kauli yake kwa kusema hali kama hiyo haikushuhudiwa wakati mbunge mteule wa Bunge la Afrika Mashariki(EALA) Dkt Oburu Oginga, ambaye ni kake mkubwa Bw Odinga alipojitokeza na kumtaka nduguye kuwa makini na uhusiano wake na Rais Uhuru Kenyatta kutokana na kupunguzwa kwa kasi ya vita dhidi ya ufisadi.

“Wakati Bw Orengo alizungumza kuhusu handsheki, alivamiwa kwa matamshi makali na Bw Mbadi na viongozi wengine wa ODM. Hata hivyo, hatujaona Dkt Oginga akivamiwa na hilo linaonyesha kuna ubabe wa nani ‘anapendeza’ Bw Odinga kwa sababu wanafahamu wakimpinga Dkt Oginga basi hawana lao mbele ya Waziri huyo Mkuu wa zamani,” akaongeza Bw Andati.

Hata hivyo, Bw Sifuna pia amelaumiwa kwa kuongoza chama kwa kujitapa na kushtumu wapinzani bila kushauriana na wenzake jinsi alivyokuwa akifanya Gavana wa Kisumu Prof Anyang’ Nyong’o ambaye alihudumu kama Katibu Mkuu wa ODM tangu kibuniwe hadi mwaka wa 2014.

Mhadhiri wa kisiasa wa Chuo Kikuu cha Maseno Dkt Tom Mboya hata hivyo anasema tofauti kubwa ndani ya ODM ni kati ya Bw Mbadi na Orengo na zinatokana na falsafa zinazokinzana za viongozi hao wawili.

“Orengo amekuwa mtetezi sugu wa Raila Odinga na siasa zake za utetezi dhidi ya uongozi wa kiimla tangu zamani ndizo zinazomwongoza kufanya kila juhudi kuhakikisha Bw Odinga anaingia Ikulu ili kurekebisha masuala ambayo yameathiri raia miaka ya nyuma.

Bw Mbadi naye amepanda ngazi kisiasa kutokana na uaminifu wake kwa Bw Odinga, ndiyo maana yupo tayari kumtetea kiongozi huyo kufa kupona dhidi ya madai yanayoonyesha anatumia muafaka na Rais kujivumisha 2022,” akasema Dkt Mboya.

Hata hivyo, ametetea Bw Mohamed kutokana na kutokuwepo kwake kwenye kampeni za Ugenya akisema huenda uhusiano wake wa karibu na Bw Odinga na uwepo wake wakati wa handsheki kulimpelekea kutoonekana kwenye mikutano iliyojaa matamshi yaliyomlenga Naibu Rais William Ruto.

“Wajua cheche za maneno makali dhidi ya Naibu Rais Dkt William Ruto ndizo zilitawala kampeni za Ugenya. Kwa kuwa Bw Odinga hakuhusika uwepo wa Bw Mohamed ungeonyesha kiongozi huyo wa ODM alikuwa akiunga mkono matamshi ya kuwasilishwa kwa hoja ya kumtimua Dkt Ruto kama Naibu Rais,” akaongeza Dkt Mboya.

Ingawa hivyo, anasema Bw Sifuna amefuata nyayo za Prof Nyong’o na kuipa chama sura ya vijana lakini akaonya kwamba anafaa kushauriana na viongozi wengine kabla ya kutoa matamshi kuhusu masuala ya kitaifa.

You can share this post!

Walimu watishia kususia mafunzo kuhusu mtaala

JAMVI: Atwoli amepiga jeki azma ya Joho kuingia Ikulu...

adminleo