Habari MsetoSiasa

Mbunge apinga pendekezo la chama kipya Pwani

April 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES LWANGA

MBUNGE wa Magarini Michael Kingi amepinga wito wa viongozi kujiunga na Chama cha Umoja Summit Party of Kenya (USPK) bila ya kuzingatia umoja wa wakazi wa Pwani kabla ya siasa za 2022.

Alizungumza baada ya katibu mkuu wa chama cha USPK Naomi Cidi kusihi wakazi wakienzi na kujiunga na chama hicho cha Pwani ili wakitumie kama daraja katika siasa za 2022.

Akizungumza katika matanga ya Gahaleni mjini Malindi ambayo yalihudhuriwa na Gavana wa Kilifi Amason Kingi, aliyekuwa mbunge wa Malindi Willy Mtengo na madiwani, mbunge huyo alisema wana majukumu makubwa ya kuunganisha wakazi wa Pwani yanayoshinda wito wa kujiunga na chama hicho.

“Kama mnadhani kujiunga katika chama ni muhimu kuliko kuunganisha wakazi wa eneo la Pwani, basi simamisheni mgombeaji katika uchaguzi mdogo wa Ganda na mjionee jinsi ataanguka. Msianzishe kitu halafu mkiachie katikati,” alisema.

Hata kabla ya kuundwa kwa chama cha USPK mwaka jana, pamekuwa na vyama mbalimbali ambavyo vimekosa kupata umaarufu na ufuasi kama vile Shirikisho Party (SPK), Kadu Asili, Chama Cha Uzalendo (CCU) na Federal Party of Kenya (FPK).

Bw Kingi alisema eneo hilo linaheshimu chama cha ODM sana na licha ya chama hicho kuwa na mizizi ya bara, wakazi wa Kilifi walikipigia kura kwa asilimia 96 katika uchaguzi mkuu uliopita ikilinganishwa na eneo la Nyanza.

“Nina imani ya kuwa eneo la Pwani linaweza kutoa rais wa nchi hii ingawa bado kuna watu wachache ambao hawaamini haya,” alisema na kuongeza kuwa “tumezoea kukaribisha wageni kila wakati na kuwachinjia kuku.”

Alisema wakati huu mtindo huo unafaa kubadilika ili wageni wakija wapate wamechinjia kuku akimaanisha kuwa watajisimamia wenyewe kisiasa katika chama cha Pwani.

Wakati huo huo, alimpigia debe kakaye mkubwa, Gavana Amason Kingi kama kiongozi wa jamii ya Mijikenda ambaye ataongoza kampeni za kuunganisha Wapwani.