Makanisa yasisitiza uchaguzi wa 2017 wafaa kutathminiwa
Na LEONARD ONYANGO
VIONGOZI wa kidini sasa wanataka tathmini ya uchaguzi wa 2017 kufanywa ili kuwe na mabadiliko yatakayohakikisha kuwa chaguzi zijazo zinakuwa huru za haki.
Viongozi hao wakiongozwa na kiongozi wa Baraza la Makanisa Nchini (NCCK) Canali Peter Karanja, walisema kuna mengi ya kujifunza kutokana na uchaguzi wa Agosti 8 na ule wa Oktoba 26 mwaka 2017.
Walipendekeza kwamba badala ya wanasiasa kuchukulia kuwa suala hilo limepita, kuwe na uchunguzi wa kina ili kuwezesha Wakenya kutambua kasoro zilizojitokeza, ili zirekebishwe.
Kwenye taarifa iliyosomwa kwa zamu baada ya kongamano la siku mbili katika jumba la Ufungamano jijini Nairobi, viongozi hao wakiwemo Askofu Martin Kivuva wa Kongamano la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (KCCB), walisema tathmini hiyo itaiwezesha nchi kurekebisha sheria za uchaguzi ili kuimarisha chaguzi za siku za usoni.
Wengine waliosoma taarifa hiyo ni Dkt Alfred Marundu wa kanisa la SDA, SB Varma (Baraza la Wahindu), Abdalla Kamwana wa Baraza Kuu la Waislamu (SUPKEM), Askofu John Warari (Evangelical Alliance of Kenya), Sheikh Muhammad Khan (National Muslim Leaders Forum) na Askofu Joseph Mutia (Organisation of African Insititued Churches).
Walisema kufanya hivyo itakuwa hatua muhimu ya kuleta utangamano, baada kuzuka kwa mgawanyiko mkubwa miongoni mwa Wakenya kwa misingi ya kikabila.
“Ili kumaliza mjadala kuhusiana na uchaguzi wa 2017, kuna haja ya kuchukua hatua ya kijasiri zitakazosaidia kuwaunganisha Wakenya na kudumisha amani.
Hatua hizo ni pamoja na kuchunguza kwa kina uchaguzi wa 2017 na kubaini mianya ambayo itazibwa ili tuwe na chaguzi za kuaminika katika siku zijazo,” akasema Askofu Kivuva.
Viongozi hao wa kidini pia walikosoa utendakazi wa maafisa wa polisi baada na kabla ya uchaguzi wa Agosti 8 na Oktoba 26 huku wakilaumu serikali kwa kujikokota kutekeleza mageuzi katika Idara ya Polisi.
Inajikokota
“Serikali inajikokota katika kufanikisha mageuzi katika idara ya polisi. Tunafaa kuwa na mdahalo wa kitaifa kuhusiana na magezi haya,” akasema Sheikh Khan.
Idara ya Polisi ililaumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji wa muungano wa National Super Alliance (NASA) waliokuwa wakipinga matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8.
Makundi ya kutetea haki za kibinadamu yalidai kuwa polisi waliua kwa risasi zaidi ya watu 30 wakati wa maandamano hayo. Lakini madai hayo yamepingwa na idara ya polisi.
“Maafisa wa polisi wanafaa kuwa na utu na kuhudumiwa Wakenya wote bila kuwa na upendeleo kwa misingi ya vyama,” akasena Sheikh Khan.
Walisema kuna haja ya kufanyia mabadiliko Katiba ili kujumuisha vipengee vitakavyounganisha Wakenya kabla na baada ya uchaguzi.
Baraza la (NCCK) limekuwa likishinikiza kupanuliwa kwa serikali na kubuni nyadhifa za Waziri Mkuu, Kiongozi wa Upinzani ili kuhakikisha kuwa wawaniaji maarufu wananufaika hata baada ya kupoteza uchaguzi.