• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Miaka 3 baada ya kuzinduliwa, Equitel yazidi kupepea

Miaka 3 baada ya kuzinduliwa, Equitel yazidi kupepea

Na BERNARDINE MUTANU

Apu ya pesa ya Benki ya Equity, Equitel, imerekodi ukuaji wa asilimia 73 kulingana na shughuli za kibiashara zilizoongezeka 2018.

Data kutoka kwa Mamlaka ya Mawasiliano (CA) inaonyesha kuwa mfumo wa Equitel ulitumiwa mara 106 milioni kufikia mwishoni mwa Desemba 2018, kutoka mara 65.9 milioni kipindi hicho 2017.

Thamani ya biashara biashara katika mfumo huo iliongezeka hadi Sh449.2 bilioni, ongezeko la asilimia 73 kutoka Sh258.9 bilioni zilizopitishwa humo katika kipindi hicho 2017.

“Ukuaji wa biashara ya Equitel umepandishwa na wauzaji rejareja wengi waliojiandikisha pamoja na wafanyibiashara wa mitandao,” alisema Meneja Mkurugenzi wa Finserve, kampuni inayoendesha huduma hiyo, Jack Ngare katika taarifa.

“Tunaendelea kushirikiana na wafanyibiashara kuhakikisha kuwa tumeanda huduma ambayo ni laini na kutoa chaguo zaidi kwa wateja,” alisema.

Kiwango cha watu binafsi waliotumia mfumo huo kutuma au kupokea fedha kiliongezeka kwa asilimia 21 kufikia Sh122.9 bilioni.

Kwa jumla, watu na mashirika yalitumia mfumo huo mara 166.4 milioni kutoka mara 110.5 kufikia ongezeko la asilimia 51 ilhali thamani ya jumla ya biashara hiyo iliongezeka kwa asilimia 33 na kufika Sh467.2 bilioni kutoka Sh350.5 bilioni.

Watu 2.075 milioni kufikia Desemba 2018 walikuwa wakitumia mfumo wa Equitel.

Mfumo huo ulianzishwa Julai 2015 na ulichangia asilimia 22 au Sh467.2 bilioni kati ya Sh2.1 trilioni zilizotumwa au kupokelewa kwa njia ya simu kufikia Desemba 2018.

You can share this post!

EABL yatangaza kuongeza bei ya pombe

Tutaendelea kupokea pesa za wanasiasa, Askofu aapa

adminleo