• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Waliofariki Sri Lanka kwa mashambulizi wafika 300

Waliofariki Sri Lanka kwa mashambulizi wafika 300

Na MASHIRIKA

IDADI ya watu waliofariki nchini Sri Lanka kutokana na msururu wa mashambulio ya bomu mnamo Jumapili imefikia 300, wamesema maafisa wa serikali.

Waliofariki walikuwa 200, lakini miili zaidi ikapatikana kwenye vifusi vya hoteli za kifahari zilizoshambuliwa.

Zaidi ya hayo, wale waliojeruhiwa pia wamefikia zaidi ya 500, huku mashirika ya uokozi yakisema kuwa huenda idadi hiyo ikaongezeka zaidi.

Shambulio hilo linakisiwa kuwa baya zaidi tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo miaka 10 iliyopita.

Milipuko hiyo ilizilenga hoteli nne maarufu jijini Colombo ambazo ni Shangri-La, Kingsbury na Cinnamon Grand na makanisa kadhaa.

Karibu waathiriwa wote wa shambulio hilo ni raia wa Sri Lanka.

Raia kadhaa wa kigeni pia walifariki. Kufikia sasa, hakuna kundi lolote ambalo limedai kuhusika katika shambulio hilo.

Jumatatu, Waziri wa Afya Rajitha Senarathe alisema kuwa mnamo Aprili 9 mkuu wa polisi nchini humo aliandika barua akionya kuhusu uwezekano wa shambulio la kigaidi.

Kwenye barua hiyo, mkuu huyo aliwaomba polisi na maafisa wengine kuimarisha usalama, hasa kwa maafisa wakuu wa serikali.

Waziri alisema kuwa baraza la mawaziri lilipata ripoti hizo baada ya mashambulio hayo kutokea.

Tayari, Rais Maithripala Sirisena ameteua kamati maalum ya watu watatu itakayoongozwa na jaji mmoja mstaafu ili kuchunguza mashambulizi hayo.

Jaji Vijith Malalgoda ndiye atakayeongoza kamati hiyo, akisaidiwa na mainspekta jenerali wa polisi N K Ilangakoon na P Jayamanna.

Afisa mmoja wa kijasusi wa Sri Lanka alisema mashambulio saba yalitekelezwa na washambuliaji wa kujitoa mhanga.

Asasi za ujasusi kufeli

Polisi pia wameanza uchunguzi kubaini ripoti kuwa asasi za ujasusi zilifeli kutekeleza onyo kadhaa zilizopewa kabla ya kutokea kwa shambulio hilo.
Mamlaka nchini humo pia zimeondoa kafyu iliyokuwa imewekwa baada ya shambulio hilo.

Kufikia Jumatatu asubuhi, barabara nyingi jijini Colombo hazikuwa na watu.

Maduka mengi yalikuwa yamefungwa, huku wanajeshi waliojihami vikali wakipiga doria kila mahali.

Baada ya mashambulio hayo, maafisa wa usalama walipata baadhi ya mabaki ya bomu yaliyokuwa yametegwa na washambuliaji.

Waathiriwa wamesema kuwa hakuna anayeweza kuwaondolea uchungu wanaopitia, baada ya kuachwa na wapendwa wao walioangamia.

Sinan Salahuddin, ambaye alimpoteza mjombake, Mohamed Rishard, aliwaambia wanahabari kuwa ni vigumu kwa machozi aliyo nayo kufutika.

“Alikuwa kama mzazi na rafiki mkubwa kwangu. Ni hali ngumu sana kwetu,” akasema.

Rishard alifariki kwenye shambulio la bomu lililotokea katika hoteli ya Shangri-La.

Alimiliki biashara iliyopakana na hoteli hiyo. Makundi mawili ya Kiislamu nchini humo yamekashifu vikali mashambulio hayo, yakisema hakuna mwanadamu anayepaswa kuuawa kwa msingi wa imani yake.

You can share this post!

VIDUBWASHA: Chaja inayochunga nyumba

SHANGAZI AKUJIBU: Mke wa zamani ameanza kumwandama tena

adminleo