• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Kiwango cha fedha kwa kaunti chaongezwa kwa asilimia 17

Kiwango cha fedha kwa kaunti chaongezwa kwa asilimia 17

Na BERNARDINE MUTANU

Kiwango cha fedha kilichopewa serikali za kaunti kiliongezeka kwa asilimia 17.8 kufikia Machi hadi Sh205.6 bilioni.

Kaunti ziliteseka kwa miezi miwili baada ya mwaka wa fedha kuanza bila kupewa pesa zozote na serikali ya kitaifa.

Kaunti zilikuwa zimepokea Sh174.5 bilioni katika kipindi kama hicho mwaka jana wakati serikali za kaunti zilichelewesha malipo ya watoaji bidhaa na huduma na pia kusimamisha miradi.

Katika muda wa miezi miwili kufikia Agosti, hakuna kaunti hata moja ambayo ilikuwa imepokea shilingi hata moja kati ya Sh314 bilioni zilizostahili kupokea kutoka kwa serikali ya kitaifa.

Kutokana na kucheleweshwa kwa fedha hizo, kulikuwa na changamoto kubwa za kifedha hali iliyosababisha kaunti kutatizika kulipia bidhaa na huduma kwa wakati ufaao, na kusababisha mrundiko wa madeni.

Kufikia Juni 30, 2018, kiwango cha madeni kilikuwa kimeongezeka hadi Sh108.41 bilioni. Mdhibiti wa Bajeti Agnes Odhiambo alisema hali hiyo kwa sehemu ilisababishwa na kucheleweshwa kwa fedha.

Katiba inahitaji Wizara ya Fedha kutoa fedha kwa kaunti kabla ya tarehe 15 kila mwezi.

Bi Odhiambo amehusisha deni kubwa katika maeneo ya kaunti tangazo la mapato ya juu kutoka huko na kuahidi watoaji wa huduma na bidhaa kwamba zina uwezo wa kulipa.

Alionya kuwa huenda kaunti zikaendelea kukabiliwa na changamoto za kifedha ikiwa zitaendelea kutumia pesa sana kwa kutarajia kupata pesa zaidi.

You can share this post!

Hamuel Muguro Ngugi aliaga dunia katika mazingira gani...

Gattuso kutua Newcastle Benitez akiondoka

adminleo