• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Kenya, Uingereza kushirikiana katika vita dhidi ya ugaidi

Kenya, Uingereza kushirikiana katika vita dhidi ya ugaidi

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI za Kenya na Uingereza zimesisitiza haja ya kushirikiana katika vita dhidi ya ugaidi.

Akiongea Alhamisi wakati wa sherehe ya kuzindua ujenzi wa Makao Makuu mapya ya Idara ya Polisi wa kukabiliana na Ugaidi (ATPU) mjini Mombasa, Balozi wa Uingereza nchini, Nick Hailey amesema taifa lake limejitolea kuisadia Kenya kukabiliana na uhalifu huo ili kuwalinda raia wake na Wakenya.

Amesema Uingereza inashirikiana na kuisadia Kenya katika kukabiliana na mashambulio ya kigaidi ambayo alisema ni kero ya kimataifa inayohitaji ushirikiano katika ngazi hiyo kuutokomeza.

Balozi Hailey amesema makao hayo makuu ni muhimu katika mchakato mzima wa kuharibu vituo vya magaidi na mashambulio ya kila mara katika eneo hili ambalo ni kitovu cha mafunzo ya kigaidi.

Inaaminika kuwa magaidi hao wana uhusiano wa karibu na kundi la al-Shabaab lenye makao yake nchini Somalia.

“Kero ya ugaidi imeathiri Uingereza pia. Hapa nchini imesababisha vifo vya Wakenya na Waingereza wengi hasa katika ukanda wa pwani ya Kenya. Tunajua hili ni tishio ambalo limevuka mipaka; tishio linalohitaji ubadilishanaji wa habari za kijasusi,” akasema.

Balozi Hailey amesema ushirikiano kati ya Uingereza na Kenya katika vita dhidi ya ugaidi ni moja katika ya wajibu mkuu wa nchi hiyo.

Hata hivyo, mwakilishi wa Malkia wa Elizabeth wa Uingereza amesisitiza kuwa vita dhidi ya ugaidi sharti viendeshwe kisheria.

“Hii itahakikisha kuwa magaidi hawakwepi mkono wa sheria kwa sababu ya makosa au ukosefu wa vifaa vya uchunguzi. Wapelekezi na waendesha mashtaka pia wanafaa kujenga kesi zenye mashiko katika ngazi kadha za utekelezaji wa haki,” Bw Hailey amesema.

Ujenzi wa makao hayo makuu ya ATPU umefadhiliwa na Uingereza iliyotoa kiasi cha Sh60 milioni.

Kwa upande wake mkurugenzi wa upelelezi George Kinoti ameishukuru serikali ya Uingereza kwa mchango wake na kushirikiana na Kenya katika masuala mbalimbali hasa usalama.

Kinoti amesema kupitia kwa msaada wa hapa nchini na wa kigeni kupitia ubadilishanaji habari za kijasusi, polisi wamefanikiwa kukabiliana na vitisho kadhaa vya ugaidi.

Naye Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji ambaye pia amehudhuria shughuli hiyo amesifu ujenzi wa makao hayo makuu akisema yatawasaidia polisi kukusanya ushahidi tosha dhidi ya washukiwa wa ugaidi.

Mradi huo umeratibiwa kukamilika Desemba 2019.

You can share this post!

LIVERPOOL: Taji si lao?

Aliyeaga dunia ndani ya seli Maragua azikwa

adminleo