• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Kaunti ya Machakos kulipa seneta Sh366 milioni

Kaunti ya Machakos kulipa seneta Sh366 milioni

Na BENSON WAMBUGU

SERIKALI ya Kaunti ya Machakos, imeagizwa kumlipa seneta wa kaunti hiyo, Bonface Mutinda Kabaka, Sh366 milioni kwa huduma alizotoa kwa niaba ya kaunti.

Jaji wa Mahakama Kuu Oscar Angote alisema kwamba ushahidi ulionyesha kwa Bw Kabaka alitoa huduma za uwakili kama mshauri wa masuala ya kisheria wa Gavana Alfred Mutua na baraza lake la mawaziri kwa miaka mitatu.

Serikali ya Kaunti ilikuwa imekanusha madai kwamba iliajiri kampuni ya mawakili ya Kabaka and Associates kukusanya ada za kima cha Sh4.8 bilioni kutoka Kapiti Plains. Serikali hiyo iliomba mahakama kuagiza idara ya upelelezi wa jinai kuchunguza kesi hiyo kubaini iwapo stakabadhi zilizowasilishwa na kampuni zilikuwa ghushi.

Mahakama iliambiwa kwamba Bw Kabaka hakuweza kuwakilisha serikali kupitia kampuni kwa sababu wakati huo alikuwa kaimu mshauri wa masuala ya sheria wa kaunti.

Kaunti ilidai Bw Kabaka alivunja sheria iwapo aliwasilisha kesi bila maagizo. Jaji Angote alisema hata kama Bw Kabaka alikuwa mfanyakazi wa Kaunti, barua ya kumwagiza kukusanya ada iliyoandikwa Julai 25 2014, siku chache kabla ya kuandikwa kwa barua yake ya kazi.

Jaji alisema aligundua kwamba barua yake ya kazi ilimruhusu kuendelea na kazi yake ya uwakili bali na huduma alizokuwa akitoa kwa kaunti kama mshauri wa masuala ya kisheria.

“ Kwa hivyo, haikuwa kinyume cha sheria, Bw Kabaka kuwasilisha kesi Agosti 18 2015 akiwa mshauri wa kisheria na mwanamikakati wa serikali ya kaunti,” alisema Jaji Angote.

Mahakama ilisema ni lazima serikali ya kaunti ilipe pesa hizo kulingana na sheria ya malipo ya mawakili.

You can share this post!

Kidero alia EACC ilimnasa kimakosa

Serikali yafufua mpango wa kufunga kambi ya Dadaab

adminleo