• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
JAMVI: Kimya cha wandani kimemwacha Ruto pweke katika safari yake ya 2022

JAMVI: Kimya cha wandani kimemwacha Ruto pweke katika safari yake ya 2022

Na WANDERI KAMAU

KIMYA cha wandani wa karibu wa Naibu William Ruto kwenye mchakato wa urithi wa Rais Uhuru Kenyatta kimeibua hofu kwamba anapigana vita hivyo peke yake.

Waandani hao, wakiwemo Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Aden Duale, Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen, Spika wa Seneti Ken Lusaka, Naibu Spika wa Seneti Kithure Kindiki na wengine, wamebaki kimya licha ya kuwa watetezi wake wakubwa, hali ambayo imeibua maswali.

Kinyume na ilivyokuwa awali, wanasiasa hao hawajakuwa wakiandamana naye katika hafla za kisiasa, wala kumtetea kutokana na mawimbi ya kisiasa yanayomkabili, hali ambayo imezua maswali.

Wachanganuzi wanasema kuwa kimya hicho si cha kawaida, ikizingatiwa kuwa viongozi hao huwa kama “jeshi lake” ambalo humtetea kila wakati anapokumbwa na mawimbi ya kisiasa.

“Ukimya huo una ufiche fulani kwani kimsingi, washirika hao waliwekwa hao kimakusudi ili kumsaidia kwenye safari yake ya kujitayarisha kuwania urais mnamo 2022. Wote ni waandani wake muhimu, lakini wamenyamaza ghafla,” asema Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Wachanganuzi wanasema kuwa kikawaida, sauti za wanne hao zinapaswa kusikika, ikizingatiwa kuwa ushirikiano wao na Dkt Ruto ulianza kitambo, wakijulikana kama “Sky Team.”

Hata hivyo, wanasema kuwa huenda kimya chao kikachangiwa pakubwa na hatua ya serikali ya kitaifa kuwanyang’anya walinzi baadhi ya washirika wa Dkt Ruto katika Mlima Kenya, maarufu kama “Team Tanga Tanga.”

Wiki iliyopita, viongozi kadhaa wakiwemo Gavana Ferdinard Waititu (Kiambu), wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Kimani Ichungwa (Kikuyu), Seneta Susan Kihika (Nakuru) kati ya wengine walinyang’anywa walinzi wao katika hali tatanishi.

Kando na hayo, magavana kumi wa ukanda wa Mlima Kenya wamekuwa wakikwepa kuhudhuria hafla za Dkt Ruto katika ukanda huo, wakisema kuwa hajakuwa akitimiza ahadi na miradi ambayo amekuwa akiahidi kwenye ziara hizo.

Magavana hao ni Francis Kimemia (Nyandarua), Ann Waiguru (Kirinyaga), Ndiritu Muriithi (Laikipia), Muthomi Njuki (Tharaka Nithi), Mwangi wa Iria (Murang’a), Mutahi Kahiga (Nyeri), Kiraitu Murungi (Meru) na Martin Wambora (Embu).

Wachanganuzi wanasema kuwa hatua ya baadhi ya viongozi kukwepa hafla za Dkt Ruto inatokana na hofu yao kutoonekana kukaidi agizo la Rais Uhuru Kenyatta kutofanya kampeni za 2022.

Kulingana na Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa, kupokonywa kwa walinzi kwa wabunge wa mrengo wa ‘Tanga Tanga’ ni dhihirisho tosha kwamba serikali inafuatilia shughuli zao kwa ukaribu.

“Kwa kuwanyang’anya walinzi, kile kilidhihirika ni kuwa rais sasa ameanza kutumia asasi za serikali kama zile za usalama kuwakabili wale wanaoonekana kukiuka maagizo yake. Ni hali ambayo bila shaka iliwafanya viongozi wengi kutathmini mielekeo yao ya kisiasa,” asema Prof Munene.

Wachanganuzi wanaonya kuwa kwa kukwepwa na baadhi ya magavana, hasa, katika ukanda wa Mlima Kenya, Ruto atakuwa na wakati mgumu kubuni kundi la viongozi ambao watamsaidia kuendelea kampeni zake, japo kichinichini ielekeapo 2022.

“Nadhani vita vya kisiasa vilivyo mbele ya Dkt Ruto ni vikubwa sana. Uchaguzi wa 2022 unaonekana kuwa kibarua kigumu kwake kadiri siku zinavyosonga. Hiki ni kinyume na 2017, ambapo alitumia ushawishi wake kuchangia kuchaguliwa kwa viongozi ambao wangemsaidia kupenya kisiasa katika ngome zote za Chama cha Jubilee (JP) kwenye kampeni zake,” asema Prof Munene.

Ijapokuwa hawajajitokeza waziwazi kueleza misimamo yao ya kisiasa, magavana wengi wa Mlima Kenya wamekuwa wakihudhuria mikutano ya kujadili masuala ya kiuchumi, wakisisitiza kuwa lengo lao kuu ni kuungana na Rais Kenyatta kutimiza Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.

“Tumegundua kuwa hitaji kuu la watu wetu ni maendeleo, badala ya siasa. Hilo ndilo jambo pekee litakalowasaidia kuinua maisha yao. Wakati wa uchaguzi, ambapo wataamua viongozi watakaowachagua kulingana na utendakazi wao,” akasema Bi Waiguru, kwenye mahojiano.

Mara tu baada ya uchaguzi, Bi Waiguru alikuwa miongoni mwa viongozi ambao walikuwa wakimkaribisha Dkt Ruto kwenye ziara nyingi alizokuwa akifanya katika Kaunti ya Kirinyaga. Kwa wakati mmoja, alisusia mojawapo ya ziara yake, akisema kwamba hakuwa amepewa mwaliko rasmi.

Wachanganuzi wanatabiri kuwa itabidi Dkt Ruto kubadili mikakati yake ya kisiasa, kwani kimya cha wandani wake huenda kikawa na athari kubwa sana kisiasa kwake.

“Ni kiongozi shupavu mwenye tajriba kubwa kisiasa. Hata hivyo, lazima mikakati yake isionekane kusambaratisha mipango ya maendeleo ya Rais Kenyatta, ambaye ndiye mkubwa wake. Wengi wanaonekana kumwacha ili kutoonekana kukaidi agizo la Rais,” asema wakili Kiprotich Mutai, ambaye pia ni mchanganuzi wa siasa.

Licha ya hayo, baadhi ya wabunge wa Bonde la Ufa wamesema kuwa watafanya kila wawezalo kuona kuwa Dkt Ruto anatimiza ndoto yake licha ya vikwazo vinavyomkabili.

You can share this post!

JAMVI: Je, Uhuru anamuandaa Gideon Moi?

JAMVI: Sababu za Uhuru kuogopa kuitisha kikao Jubilee

adminleo