Tobiko aunda jopokazi la kulinda misitu
Na BERNARDINE MUTANU
WAZIRI wa Mazingira Keriako Tobiko ameunda jopokazi la kusimamia misitu nchini.
Miongoni mwa wanakamati wa jopo hilo ni watu walio na utaalam mkubwa katika masuala ya mazingira.
Jopo hilo linalenga matokeo ya haraka katika usimamizi wa misitu hasa ukataji wa miti na usimamizi wa rasilimali ya misitu.
Kulingana na taarifa kutoka kwa Wizara ya Mazingira, jopo hilo linalenga kubainisha kiwango cha uharibifu wa mazingira nchini.
Inaonekana waziri huyo ameunda jopo hilo baada ya malalamishi mengi kuhusiana na athari za uharibifu wa misitu nchini.
“Jopo hilo litapendekeza njia za kuhakikisha kuwa misitu imerudi kwa njia endelevu,” ilisema taarifa hiyo.
Litasimamiwa na mwenyekiti wa Shirika la Green Belt Movement, Marion Wakanyi Kamau na naibu mwenyekiti wa Taasisi ya Kitaifa ya Mazingira Bi Linda Munyao,
Wengine ni Christian Lambrechts (Mkurugenzi Mkuu wa Wakfu wa Rhino Ark), Bi Phyllis Wakiaga (Mkurugenzi Mkuu wa Kenya Association of Manufacturers (KAM) na Mwenyekiti wa Shirika la Kenya Water Towers Agency Bw Isaac Kalua.
Adil Khawaja (Mkurugenzi KCB), Duncan Kimani(KEPSA), Ernest Nadome(COTU) na mawakili Faith Waigwa na Gideon Kilakoi.
Ripoti ya mwanzo ya jopo hilo inatarajiwa katika muda wa siku 14, alisema Bw Keriako Tobiko.