Msanii Chameleone azuiwa kumuona Bobi Wine gerezani
Na DAILY MONITOR
JUHUDI za mwanamuziki maarufu nchini Uganda Joseph Mayanja, maarufu Jose Chameleone, kumtembelea mbunge wa Kyadondo Mashariki Robert Kyagulanyi anayezuiliwa katika gereza la Luzira, ziliambulia patupu baada ya kutimuliwa na polisi.
Kyagulanyi, almaarufu Bobi Wine alikamatwa Jumatatu na kuzuiliwa rumande kwa madai ya kupuuza sheria mnamo Julai 11, 2018 alipokuwa akipinga ushuru unaotozwa wanaotumia mitandao ya kijamii.
Chameleone jana alisema kuwa alitimuliwa na polisi kutoka gerezani hapo kwa sababu hakupewa idhini na Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Magereza Johnson Byabasaija kwenda kumwona mwanamuziki mwenzake Bobi Wine.
“Leo asubuhi niliamka na kwenda katika gereza la wahalifu sugu la Luzira kumtembelea mwanamuziki mwenzangu, Bobi Wine. Nilipofika niliambiwa nilifaa kupata ruhusa kutoka kwa kamishna wa magereza.
“Nilijaribu kuwashawishi waniruhusu nikutane na Bobi Wine lakini wakakataa. Hata hivyo, nakuombea ndugu yangu,” akasema Bw Chameleone.
Chameleone alikuwa ameandamana na Meya wa Kampala Erias Lukwago, mbunge wa Mityana Francis Zaake, mbunge wa Mukono Municipality Betty Nambooze na mwanamuziki mwenzake Nubian Li.
Chameleone alizuru gereza hilo saa chache baada ya maafisa wa polisi kuwatawanya kwa vitoa machozi waandamanaji waliojitokeza kupinga kukamatwa kwa Bobi Wine.
Mamia ya watu walijikusanya katika mitaa mbalimbali jijini Kampala siku moja baada ya mwanasiasa huyo kutiwa mbaroni.
Idara ya polisi ilitoa taarifa ikidai kuwa waandamanaji hao walitawanywa walipojaribu kuzua vurugu.
Waandamanaji hao walichoma magurudumu katikati mwa barabara na kutatiza shughuli za usafiri wakati wa maandamano hayo.
Bobi Wine alikamatwa siku mbili baada ya kuzuiliwa na polisu kutoka kwake kwa siku mbili.
Alikamatwa alipokuwa akielekea katika tamasha la muziki katika ukumbi wake wa One Love Beach ulioko eneo la Busabala wilayani Wakiso.
Mbunge huyo leo anatarajiwa kujua hatima yake iwapo ataachiliwa huru au la.
Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Amnesty International limeitaka serikali ya Uganda kumwachilia huru Bobi Wine.