Wakenya wanaamini vyombo vya habari – Ripoti
Na WANDERI KAMAU
WAKENYA wengi wanaviamini vyombo ya habari kwa kuangazia masuala muhimu yanayoikumba nchi, imeonyesha ripoti mpya.
Ripoti hiyo, ambayo ilitolewa na Baraza la Vyombo vya Habari (MCK) kwa ushirikiano na shirika la utafiti la Infotrak, inaonyesha kuwa karibu robo ya wananchi wanaviunga mkono kwa kuripoti masuala hayo.
Masuala mengine yaliyoibukia kupendelewa ni uangaziaji wa habari za mashinani, habari zinazochipukia, ufuatiliaji wa habari muhimu, umaarufu wa wanahabari mbalimbali, uhuru wa habari zinazopeperushwa na uangaziaji wa watu maarufu.
Kwa mara nyingine, Wakenya zaidi wangali wanaviamini vyombo vya habari kama mojawapo ya taasisi zinazoaminika.
Utafiti ulionyesha kuwa zaidi ya nusu ya Wakenya wanaviamini vyombo hivyo kama asasi inayoaminika zaidi.
Kando na hayo, televisheni ziliibuka kama vyombo vinavyotegemewa na Wakenya wengi, zikifuatwa na redio, mitandao ya kijamii na magazeti.
Na huku mitandao ya kijamii ikiendelea kuwa maarufu miongoni mwa Wakenya, robo ya waliohojiwa walisema huwa wanaitumia kubuni urafiki na watu wengine.
“Kuibuka kuwa watu wengi wanaotumia mitandao hiyo kubuni urafiki inaonyesha kuwa watu wanaanza kutambua umuhimu wa matumizi yake katika maisha yao ya kila siku,” ikasema ripoti.
Kando na kubuni urafiki, mitandao ya kijamii pia iliibuka kama mihimili muhimu kwa Wakenya kupata habari.