• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
CBK yaonya benki kuhusu wafanyakazi walaghai

CBK yaonya benki kuhusu wafanyakazi walaghai

Na BERNARDINE MUTANU

Benki Kuu ya Kenya (CBK) imezitaka benki kuimarisha ukaguzi wa wafanyikazi wake na biashara za nje. Hii ni kutokana na ongezeko la udanganyifu.

Gavana wa CBK Patrick Njoroge Ijumaa alisema benki hazifai kusahau kuwa tishio nyingi dhidi ya wateja wao kupitia kwa mitandao na mifumo huanzishwa na wafanyikazi wake au watu wengine wanaoweza kuingilia mifumo yake.

“Benki zinapokabiliana na masuala ya wateja, zinafaa kukagua kwa makini kuhakikisha kuwa zimezuia uvamizi wa kimfumo na mitandao ndani. Zinafaa kuhakikisha wafanyikazi wake hawageuki kuwa mzigo,” alisema Dkt Njoroge.

“Kumekuwa na ongezeko la uvamizi wa kimitandao na mifumo unaoongozwa au kusaidiwa na wafanyikazi, hivyo, kuna haja ya kuhakikisha kuwa wafanyikazi wamechunguzwa vilivyo,” alisema.

Alisema hayo alipohudhuria hafla ya Chama cha Wamiliki wa Benki (KBA) ya kuzindua kampeni ya #KaaChonjo inayolenga kuwahelimisha wateja dhidi ya kuepuka udanganyifu na tishio la udanganyifu.

Dkt Njoroge alisema uchunguzi wa kina wa wafanyikazi wakati wa kupewa ajira utasaidia kuzuia wadanganyifu.

Aliomba benki kutofautisha majukumu vyema na kuzindua programu za kudhibiti hatari ya uvamizi.

Benki siku hizi zinapata huduma kutoka nje kwa lengo la kuimarisha uzalishaji. Hata hivyo, hatua hiyo pia inaongeza hatari, alionya msimamizi huyo wa CBK.

Alizitaka pia kukagua kampuni za utoaji huduma kabla ya kuzipa kazi.

You can share this post!

Madaktari wa Cuba wahamishiwa kaunti zingine

Tullow kuanza kuchimba mafuta baada ya kupata idhini ya NEMA

adminleo