• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 10:55 AM
Kenya yatafuta msaada wa ulinzi katika Pentagon

Kenya yatafuta msaada wa ulinzi katika Pentagon

Na VALENTINE OBARA

SERIKALI ya Kenya imefanya mashauriano na Wizara ya Ulinzi ya Amerika, maarufu kama Pentagon, kwa lengo la kupokea usaidizi wa kuimarisha usalama wa nchi.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Bi Monica Juma alikutana Jumanne na maafisa wa Pentagon na wakajadiliana kuhusu jinsi mataifa hayo mawili yanaweza kushirikiana kuimarisha usalama nchini na vile vile, barani Afrika kwa jumla.

Kulingana na Bi Juma, ushirikiano katika masuala ya ulinzi ambao umekuwepo kati ya Kenya na Amerika kwa miaka mingi sasa ni wa kupigiwa mfano kwa kuwa umesaidia pakubwa kuchangia katika uboreshaji wa usalama na amani kimataifa na unastahili kudumishwa.

Aliongeza kwamba, hakutakuwa na manufaa yoyote kwa nchi hizo mbili kushauriana kuhusu jinsi zinavyoweza kushirikiana kustawisha uchumi, uwekezaji na uongozi bora bila kuboresha usalama.

“Ugaidi ni tishio kubwa zaidi kwa ufanisi wa ushirikiano wetu kwa vile hata kama tutakuwa na maono makubwa ya kimaendeleo na kuwekeza kwa mandhari bora ya kuvutia uwekezaji, lazima tukabiliane na ugaidi la sivyo kutakuwa na hatari ya kutofanikiwa katika malengo yetu,” akasema.

Alikuwa akizungumza jijini Washington, Amerika ambapo anaongoza ujumbe wa Kenya katika ziara inayolenga kukuza ushirikiano mwema kati ya Kenya na Amerika.

Miongoni mwa walioandamana naye katika ziara hiyo ni Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i ambaye pia ni Mshirikishi wa Shughuli za Serikali, pamoja na maafisa wakuu kutoka wizara nyingine mbalimbali.

Ziara hiyo iliandaliwa kufuatia makubaliano ya Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Amerika, Donald Trump mnamo Agosti mwaka uliopita kutafuta namna ya kukuza ushirikiano wa mataifa hayo mawili.

Masuala mengine makuu yanayoangaziwa ni kuhusu uchumi na uwekezaji, demokrasia, uongozi bora na masuala yanayohusu bara zima la Afrika.

Bi Juma na Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni Amerika, Bw John Sullivan walitia saini mwongozo utakaosimamia mashauriano kati ya nchi hizo mbili kuanzia sasa.

“Mwongozo huu ni sharti usaidie kuleta mali kwa watu wetu, ulete nafasi za ajira, maisha bora na uchangie katika kustawisha nchi yetu na ulimwengu kwa jumla.

Lazima pia tutie bidii kuhakikisha Afrika iko salama kwa uwekezaji kupitia kwa utulivu wa kisiasa, uhuru wa kidemokrasia na tuhakikishe pia kwamba, tuko huru kutokana na kila aina ya vitisho, hasa ugaidi,” akasema Bi Juma.

Kwa upande wake, Bw Sullivan alisifu mkutano huo kama ishara ya jinsi Kenya na Amerika zilivyojitolea kutekeleza majukumu makubwa yatakayochangia ufanisi wa kimataifa.

“Kenya ni mojawapo ya washirika wetu wakuu ulimwenguni,” akasema Bw Sullivan.

Kwa miaka mingi, Amerika imekuwa ikichukulia Kenya kwa umuhimu mkubwa kutokana na jinsi taifa hili linavyochangia pakubwa katika utekelezaji wa malengo makuu ya kimaendeleo Afrika ikilinganishwa na mataifa mengine hasa ya Afrika Mashariki.

Kwa sasa, wafanyabiashara kutoka Amerika wanalenga kuwekeza katika ujenzi wa miundomsingi mikuu nchini.

You can share this post!

Wakazi waponea ukuta wa jumba ukiporomoka

MUTANU: Visa vya mauaji miongoni mwa vijana vichunguzwe kwa...

adminleo