Chifu kizimbani kwa kuiba mbwa!
JOSEPH WANGUI Na PETER MBURU
CHIFU kutoka eneo la Othaya alishtakiwa katika mahakama moja ya Nyeri Alhamisi, kwa madai kuwa aliiba mbwa wawili wa mhubiri wa Nairobi Thomas Wahome Njuguna, wa kanisa la Helicopter.
Paul Gachiri Wageni, naibu chifu wa Kiandemi alituhumiwa kuiba mbwa hao wa gharama ya Sh300,000 tarehe isiyojulikana, Desemba 2016 katika kijiji cha Kihuri.
Vilevile, alishtakiwa kuwa alipatikana na mali ya wizi Desemba 6, 2018 katika kijiji hicho.
Afisa huyo, hata hivyo, alikana mashtaka na akaachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000, kesi hiyo ikiratibiwa kusikizwa Juni 4, 2019.
Nakala ambazo upande wa mashtaka unategemea zinasema kuwa mlalamishi alinunua mbwa hao Desemba 2014 Arusha, Tanzania na wakasafirishwa kwa ndege walipokuwa na miezi mitatu.
Aliwasafirisha hadi nyumbani kwake Othaya, ambapo walikuwa wakichungwa na meneja wa shamba lake Stephen Macharia, ambaye alimfahamisha kuhusu kuibiwa kwao.
“Niliripoti kisa hicho kwa naibu chifu Paul Gichiri ili atangaze wakati wa mikutano ya baraza kwani nilishuku waliibiwa na mmoja wa majirani, kisha nikarejea Nairobi nikisubiri majibu,” mhubiri huyo akaeleza polisi.
Lakini Novemba 3, 2018 meneja wa shamba lake aliripoti kuwa aliona mbwa hao nyumbani kwa chifu huyo, kisa ambacho kiliripotiwa kwa polisi Othaya.
Habari za polisi aidha zinasema kuwa meneja huyo pamoja na polisi walienda hadi nyumbani kwa chifu huyo na wakawaona mbwa hao.
Chifu huyo anadaiwa kuambia polisi kuwa aliwanunua mbwa hao kutoka kwa mamake mhubiri ambaye ni mlalamishi, mnamo Machi 2013 kwa Sh200 kila mmoja.
“Wiki mbili baada ya kuwanunua, mbwa dume alifariki na akasalia jike ambaye tangu wakati huo amezaa mara mbili,” ripoti ya chifu kwa polisi ikasema.