Habari Mseto

Collymore ateuliwa kwa bodi ya kukabili kansa

May 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mawasiliano ya Safaricom Bob Collymore sasa ni mwanachama wa bodi ya Taasisi ya Kitaifa kuhusu Kansa.

Bw Collymore aliteuliwa na Waziri wa Afya Sicily Kariuki, kuhudumu kwa muda wa miaka mitatu. Mkurugenzi huyo aliteuliwa pamoja na wengine watatu, David Makumi, mwenyekiti wa Kenya Network of Cancer Organisation, Mercy Oburu anayesimamia masuala ya kidijitali Royal Media na Dkt Evangeline Njiru.

Bw Collymore mwaka wa 2017 alichukua livu ya miezi tisa kurejea kwao Uingereza kutibiwa kansa.

Mwenyekiti wa taasisi hiyo ni Dkt Ochiba Lukandu. Kwa muda, taasisi hiyo ilikuwa haifanyi kazi na uteuzi huo umefaa zaidi kwani itaanza kufanya kazi, wakati ambapo visa vya kansa vinazidi kuripotiwa nchini.

Taasisi hiyo itakuwa na majukumu ya kudumisha sajili ya visa vya kansa, kushauri waziri kuhusiana na njia za kukabiliana na ugonjwa wa kansa ambao huuwa Wakenya 40,000 kila mwaka, na kusaidia katika usambazaji wa vifaa vya kuchunguza kansa.

“Taasisi hiyo inalenga kuimarisha sajili ya kitaifa ya kansa ambako kila hospitali, na daktari, itatakiwa kuripoti visa vipya vya kansa,” alisema Bw Makumi.

Sajili hiyo ilibuniwa chini ya Sheria ya Kuzuia na Kudhibiti Kansa 2012, ambayo imetoa adhabu kwa wote wanaokataa kuripoti visa vipya vya kansa.

Madaktari na hospitali wanaweza kutozwa hadi Sh200,000 kwa kukataa kuripoti visa vipya vya kansa au vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.