• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
YA MUSA NA FIRAUNI: Fainali ya kiajabu kati ya klabu za Uingereza

YA MUSA NA FIRAUNI: Fainali ya kiajabu kati ya klabu za Uingereza

Na MASHIRIKA

AMSTERDAM, Uholanzi

HUKU dunia ikiendelea kustaajabia ya Liverpool dhidi ya Barcelona, ulimwengu ulishuhudia maajabu mengine ya Tottenham Hotspur dhidi ya Ajax Amsterdam, chambilecho wahenga ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni.

Siku moja baada ya tukio la kugutusha uwanjani Anfield Liverpool ilipoisagasaga Barcelona, ilitokea siku nyingine ambapo machozi ya furaha na kilio yalitanda baada ya Tottenham kuibandua Ajax nje ya kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), duru ya pili, kupitia mabao matatu ya ugenini kutoka kwa raia wa Brazil, Lucas Moura.

Nusu fainali hiyo iliisha kwa jumla ya mabao 3-3 mnamo Jumatano, lakini Spurs ikafuzu kwa kanuni ya mabao (mengi) ya ugenini .

Kocha wa Spurs, Mauricio Pochettino alilia kwa furaha na kuwataja wachezaji wake kama zaidi ya mashujaa baada ya bao la Moura katika dakika ya sita ya muda wa majeruhi kukutanisha klabu za Uingereza katika fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2008.

Fainali ni Juni 1 katika uwanja wa nyumbani wa klabu ya Atletico Madrid, Wanda Metropolitano.

Ushindi huo wa dakika ya mwisho kupitia mabao ya ugenini uliwasili saa 24 baada ya Liverpool kuaibisha Barcelona 4-0.

Ajax, ambayo nahodha wake ni beki chipukizi Matthijs de Ligt, 19, ilionekana itaingia fainali ilipokuwa ikifurahia kuongoza kwa jumla ya mabao 3-2 dakika za ziada zikiyoyoma uwanjani Johan Cruyff Arena.

Kisha, Moura, ambaye aliuziwa Spurs kwa bei ya chini baada ya kutemwa na Paris Saint-Germain, akafunga bao hilo la uchungu.

Alipata mpira ndani ya kisanduku na kumwaga kipa wa Ajax, Andre Onana na kusaidia Spurs kushinda mechi ya marudiano 3-2.

“Ulikuwa usiku muhimu kabisa katika maisha yangu,” alisema Pochettino ambaye alibubujikwa na machozi ya furaha baada ya kipenga cha mwisho kulia.

“Vijana wangu walifanya kazi safi sana. Nilisema hapo awali kwamba wao ni mashujaa. Nadhani vijana wangu sasa ni zaidi ya mashujaa. Kufikisha klabu katika fainali ni karibu na kufanya muujiza.”

Moura pia alizidiwa na hisia.

“Soka inatupa fursa kama hizi ambazo hatuwezi kufikiria,” alisema.

“Tunastahili kufurahia. Hebu nitazame, huu ni wakati ambao najivunia zaidi katika maisha yangu, taaluma yangu.”

Huzuni

Wachezaji wa Ajax waliketi uwanjani kwa huzuni na kilio baada ya tiketi ya kufika fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1996 kutolewa kinywani.

Waholanzi walishinda mechi ya mkondo wa kwanza 1-0 na walionekana kuzamisha Spurs kabisa walipoongeza mabao mawili katika kipindi cha kwanza cha mechi ya marudiano kutoka kwa De Ligt na Hakim Ziyech mjini Amsterdam.

Hali hiyo iliacha Tottenham ikihitaji ufufuo sawa na ule Liverpool ilipata dhidi ya Barcelona usiku uliotangulia, lakini kwa hata muda mchache zaidi.

Mabao mawili ya haraka kutoka kwa Moura katika kipindi cha pili yalifufua matumaini ya Spurs kabla ya Mbrazil huyu kugonga msumari wa mwisho.

Vijana wa Erik ten Hag sasa hawana budi kujinyanyua kuendelea kufukuzia mataji la Ligi Kuu na Kombe nchini Uholanzi.

Timu ya Ajax huenda ikapoteza wachezaji muhimu kabla ya msimu mpya kuanza kwa sababu Frenkie de Jong tayari ameshasaini kandarasi na Barcelona naye De Ligt anamezewa mate na miamba hao wa Uhispania, ingawa Manchester United pia inaaminika kuwa mbioni kutafuta huduma zake.

Ajax na Spurs ziliingia mechi ya marudiano bila wachezaji muhimu. Mvamizi Harry Kane (Spusr), ambaye huenda akarejea katika fainali dhidi ya Liverpool, alikuwa mkekani akiuguza jeraha. Ajax nayo ilipata pigo pale winga Mbrazil David Neres aliumia kabla tu ya mechi ya marudiano kuanza.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Nilitarajia harusi baada ya miaka 3, sasa...

Waelezea jinsi wanavyofurahia maendeleo Thika

adminleo