Kimataifa

Familia sasa yamzuia mke kumtembelea Morgan Tsvangirai hospitalini

February 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Bi Elizabeth Tvangirai akihutubu awali. Picha/ Hisani

Na MASHIRIKA

HARARE, ZIMBABWE

Kwa Muhtasari:

  • Bi Elizabeth Tsvangirai analaumiwa kumuunga mmoja wa manaibu wake watatu wa chama cha MDC kurithi mumewe
  • Wanahofia kwamba huenda mwanamke huyo akamsaidia Nelson Chamisa kuwa kiongozi wa chama bila kufuata katiba
  • Elizabeth Tsvangirai aliambia Daily News kwamba atatoa taarifa mumewe akitoka hospitalini.

WATU wa familia ya kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai, wamemzuia mkewe Elizabeth, kumtembelea hospitalini baada ya kumlaumu kwa kumuunga mmoja wa manaibu wake watatu wa chama cha MDC kumrithi.

Tsvangirai anatibiwa katika hospitali ya Wits Donald Gordon Medical Centre jijini Johannesburg.
Kumekuwa na habari za kutatanisha kuhusu afya yake baadhi ya watu wakidai kwamba maisha yake yako hatarini.

 

Hofu

“Jamaa za karibu za kiongozi huyo wa chama cha MDC wanamlaumu Elizabeth kwa kumuunga mkono naibu wa kiongozi wa MDC, Nelson Chamisa kumrithi Tsvangirai na wanahofia kwamba huenda akamsaidia kuwa kiongozi wa chama bila kufuata katiba ya chama,” liliripoti gazeti la kibinafsi la Daily News.

Chamisa ni mmoja wa manaibu watatu wa kiongozi wa MDC wanaowania uongozi wa chama baada ya Tsvangirai.

Mnamo Jumatano, msemaji wa Tsvangirai alisema Chamisa alikuwa ameteuliwa kuwa kaimu kiongozi wa chama. Hata hivyo, msemaji wa chama Obert Gutu, alikanusha na kusema aliyekuwa meya wa Harare, Elias Mudzuri, angali anashikilia uongozi wa chama hicho.

Madzuri aliteuliwa kaimu kiongozi wa chama hicho Januari wakati Tsvangirai alipoondoka Zimbabwe kwenda Afrika Kusini mwa matibabu.

 

Kukutana

Kwenye ujumbe wa Twitter Ijumaa, Mudzuri, ambaye yuko Afrika Kusini, alidai alikutana na Tsvangirai na kwamba alipanga kukutana naye tena.

“Ningali kaimu kiongozi hadi atakaporejea. Tafadhali msiyumbe, endeleeni kutia nguvu chama ili kushinda uchaguzi. Puuzani habari za uongo,” alisema Bw Mudzuri.

Elizabeth Tsvangirai aliambia Daily News kwamba atatoa taarifa mumewe akitoka hospitalini.

“Kwa sasa, ninachozingatia ni ugonjwa wa mume wangu, kinachoendelea, sina la kusema,” alisema.