MakalaSiasa

JAMVI: Kauli ya Raila kuhusu SGR inamponza au inamjenga kisiasa?

May 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na BENSON MATHEKA

Kauli ya kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kuhusu mkopo wa kujenga reli ya kisasa (SGR) kutoka Naivasha hadi Kisumu ambao haukupatikana ilikuwa kosa kubwa japo huenda lisiathiri pakubwa umaarufu wake katika ngome yake ya kisiasa.

Wadadisi wanasema kauli hiyo ya Bw Odinga itakuwa kovu katika maisha yake ya kisiasa hasa wakati huu ambao umaarufu wake katika eneo la Nyanza uko kwenye mizani kufuatia kushindwa kwa chama chake kwenye uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge cha Ugenya.

Bw Odinga alikuwa amehakikishia wakazi wa Nyanza na kusini mwa Bonde la Ufa kwamba angeandamana na Rais Uhuru Kenyatta hadi China kupata mkopo wa kujenga reli ya kisasa kutoka Naivasha hadi Kisumu.

Aliwahakikishia kwamba reli hiyo ingefaidi eneo hilo pakubwa. Kauli yake ambayo alitoa kwa lugha ya mama akiwa Nyakach mnamo Aprili 20, iliwapa wakazi wa Nyanza matumaini makubwa ambayo yalididimia serikali iliposema haikujadili mkopo katika ziara ya rais China.

Ingawa serikali haikukanusha kauli yake alipoashiria kuwa ziara yake na Rais China ilikuwa ya kutafuta mkopo wa kujenga reli ya kisasa hadi magharibi mwa Kenya, baadaye ilikanusha kwamba suala hilo lilikuwa ajenda ya ziara hiyo.

Aidha, iliibuka kuwa Bw Odinga aliwakilisha Muungano wa Afrika (AU) katika kongamano ambalo Rais wa Kenya alikuwa amehudhuria kikao Beijing na hakuwa miongoni mwa ujumbe wa Kenya.

Vyombo vya habari viliporipoti kwamba Kenya ilinyimwa pesa za kujenga reli ya kisasa kutoka Naivasha, serikali ilikanusha vikali na Wakenya wakaanza kumulika matamshi ya Bw Odinga.

Wadadisi wanasema kuwa hata kama Kenya ilinyimwa mkopo huo au suala hilo halikuwa kwenye ajenda ya ziara ya rais, kauli ya Bw Odinga ilimponza kama kiongozi.

“Nafikiri lilikuwa tamko la kisiasa ambalo watu walilichangamkia ikitizingatiwa manufaa yanayotokana na mradi wa mabilioni kama huo. Japo kuna waliofurahia mkopo huo kutokapatikana, ni matarajio ya watu yanayofanya Bw Odinga kuonekana alidanganya,” asema mdadisi wa masuala ya kisiasa Peter Ouko.

Anasema huenda Bw Odinga alitoa kauli hiyo ili kuonyesha wafuasi katika ngome yake ya kisiasa wanafaidika na ukuruba wake wa kisiasa na Rais Kenyatta. Viongozi hao wawili walikuwa mahasimu wa kisiasa kabla ya kuzika tofauti zao na kuamua kushirikiana kuleta amani nchini.

Bw Ouko anasema kinachomponza Bw Odinga ni watu kugundua kwamba hakuwa kwenye ujumbe wa serikali ulioandamana na Rais Kenyatta China mbali alikuwa akiwakilisha Muungano wa Afrika.

“Binafsi ninaamini kwamba suala hilo liliibuka kwenye ziara ya Rais China lakini mkopo haukupatikana kwa sababu ambazo serikali haikutaja. Hata hivyo, watu walipobaini kwamba Bw Odinga hakuwa kwenye ujumbe wa Kenya, waliamini kauli ya serikali na kumuona kama mdaganyifu,” alisema.

Alipoulizwa afafanue matamshi yake katika kikao kimoja na wanahabari wiki hii, Bw Odinga alikataa akisema serikali ilikuwa imetoa maelezo yote kuhusu suala hilo.

Kulingana na Ikulu, habari kuhusu Kenya kunyimwa mkopo wa kujenga reli zilikuwa za kupotosha.

“Mwakilishi wa Muungano wa Afrika kuhusu miundomisingi (Odinga) alihudhuria mkutano huo akiwakilisha AU na ni jukumu lake kujadili masuala hayo,” alisema mkuu wa wafanyakazi wa Ikulu Nzioka Waita.

Kulingana na Bw Waita, Bw Odinga hakufaa kuomba radhi wa matamshi hayo kwa sababu anahusika na masuala ya miundomisingi barani Afrika.

“Nafikiri Bw Odinga anatakia nchi hii mambo mazuri lakini ukweli ni kuwa suala hilo halikuwa kwenye ajenda (ya ziara ya rais) China,” alisema.

Bw Ouko anasema ikizingatiwa akiwa mwanasiasa mweledi na anayeelewa wafuasi wake vyema, Bw Odinga anafahamu atakavyokabiliana na suala hilo likizuka siku zijazo.

“Hata kama ilichukuliwa kwamba aliandaa Wakenya kuhusu suala hilo, Odinga ni mwanasiasa ambaye anajua jinsi ya kuteka wafuasi wake na kuwafanya wasahau yaliyopita,” alisema.

Anasema hali ingekuwa tofauti iwapo serikali ingemshutumu moja kwa moja kwa kupotosha Wakenya.

“Badala ya kumshutumu serikali ilimtetea ikisema akiwa Mwakilishi wa Muungano wa Afrika kuhusu miundomisingi, ni jukumu lake kuzungumzia suala hilo. Hii ilizima joto ambalo linaweza kuvumisha hali inayomkabili hasa baada ya chama chake kushindwa katika uchaguzi mdogo wa Ugenya,” anasema Bw Ouko.

Baadhi ya wadadisi wanasema licha kutetewa na serikali, kauli hiyo inaweza kutumiwa na wapinzani wake wakati wa kampeni siku zijazo iwapo atagombea urais wakitaka kumsawiri kama mtu asiyeweza kuaminiwa.