• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
JAMVI: Ukosefu wa mrithi Mlima Kenya kunavyomfaidi Ruto

JAMVI: Ukosefu wa mrithi Mlima Kenya kunavyomfaidi Ruto

 Na PETER MBURU

TANGU Uchaguzi Mkuu wa 2017 ambapo Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto walichaguliwa kwa muhula wa pili, eneo la Mlima Kenya limekuwa likiyumba kisiasa, viongozi wake mara kwa mara wakichukua misimamo kinzani.

Tangu alipochaguliwa tena, Rais Kenyatta amekuwa kimya kuhusu masuala ya kisiasa, kila wakati akisisitiza kuwa ni wakati wa kufanya kazi na kuwa wakati wa siasa utafika, 2022.

Hali hiyo imeacha eneo la Mlima Kenya likitetereka na viongozi kuelekea pande tofauti, Rais akiachwa na viongozi wachache tu ambao wanamuunga mkono moja kwa moja.

Uhusiano baridi baina ya Rais na naibu wake aidha umewafanya viongozi wengi wa Mlimani kumfuata Dkt Ruto, wakikaidi wito wa Rais Kenyatta ambaye ndiye msemaji wa kisiasa Mlima Kenya, hata baada yake kujaribu kutumia kifua.

Wengi walikuwa wametarajia kuwa huenda Rais angetangaza mrithi wake wa kiti cha Msemaji wa jamii ya Kikuyu kwa haraka kwa kuwa hatakua debeni 2022, lakini inavyoelekea ni kuwa hilo haliji kwa haraka.

Vilevile, hakujatoka jambo lolote kutoka kwa mabwanyenye wa kibiashara wa eneo hilo, ambao kwa miaka mingi ndio wamekuwa na usemi wa mwisho kuhusu atakayekuwa msemaji wa jamii na eneo.

Kujivuta kwa Rais na mabwanyenye hao, ambao usemi wao una uzito mkubwa sasa kumewafanya viongozi kusalia kama mifugo wasio na mlinzi, kila mmoja akielekea anakoona lishe na kuanza kupuuza amri za uongozi.

Wadadisi wanahoji kuwa huenda kuchelewa sana kwa Rais ama mabwanyenye hao kufikia uamuzi kuhusu atakayepeperusha bendera ya jamii kisiasa kukaathiri siasa za eneo hilo uchaguzi ujao, na kuishia kuwafaa wapinzani.

“Kwa sasa viongozi wametawanyika vibaya na Mlima Kenya unaonekana kuwa uwanja wa viongozi kutoka maeneo mengine kufika, kuwasha moto na kujinyakulia viongozi kadha kuwaunga mkono,” anasema Yusuf Ghandhi, mdadisi wa masuala ya uongozi.

Wakati Mlima ukiteketea, Naibu Rais naye amekuwa akitumia kila mbinu kufika huko kujinyakulia viongozi, juhudi ambazo zimeonekana na wengi kama kujaribu kumhangaisha mkubwa wake, lakini maoni ya wadadisi ni kuwa akitumia fursa hii vyema, huenda akawa na cha kufurahia mwishoni.

Dkt Ruto amekuwa akifululiza eneo la Mlima Kenya katika Kaunti za Kiambu, Murang’a, Embu, Nyeri na zingine zinazohusishwa nao kama Nakuru kila wakati, matokeo yakiwa viongozi wa maeneo hayo kumfuata na kudai watamuunga mkono 2022, liwe liwalo.

Hali yake ilisababisha kujitokeza kwa makundi ya ‘Team Tangatanga’ na ‘Team Kieleweke’, japo uzito wa ‘Tangatanga’ unaonekana kuemea eneo la Mlimani.

“Hali ya Naibu Rais kuzuru Mlima Kenya kila baada ya muda mfupi inamjenga katika maeneo hayo, hasa anapofika mbele ya wananchi akiwa na viongozi wao wa ngazi za chini kama wabunge na maseneta. Ni ha li ambayo inafanya hata wananchi ambao hawakuwa wamemkubali kuanza kuwaza tena,” anasema wakili Kipkoech Ngetich.

Hadi sasa, Dkt Ruto ana uungwaji mkono kutoka kwa magavana Mwangi Wa Iria (Murang’a), Anne Waiguru (Kirinyaga), Ferdinand Waititu (Kiambu) na Mutahi Kahiga (Nyeri), maseneta Irungu Kang’ata (Murang’a) na Susan Kihika (Nakuru) na wabunge Kimani Ngunjiri (Bahati), Kimani Ichungwa (Kikuyu), Alice Wahome (Kandara), miongoni mwa wengine.

Majuzi, mbunge mwanamke wa Kaunti ya Kiambu Gathoni Wamuchomba alikiri wazi kuhusu jinsi uzito wa ‘Tangatanga’ unazidi, akidai kuwa upande wao wa ‘Kieleweke’, ambao sasa wanajiita ‘Team Kenya’ wamesalia wanne pekee.

“Na wabunge wote wa Mlima Kenya wamemwachilia Rais Kenyatta, hapa Kiambu tumebaki na (Paul) Koinange (mbunge wa Kiambaa), Naibu Gavana wetu (James) Nyoro na mbunge wa Limuru Peter Mwathi,” akasema Bi Wamuchomba.

Mwanasiasa huyo aliongeza kuwa “Sisi tutajua pa kuelekea 2022 wakati Uhuru atakapotupa mwelekeo”, wakati wenzao wanaomuunga mkono Naibu Rais kutoka eneo hilo wanazidi kuzunguka naye nchini, wakiimba wimbo wake.

Viongozi kadhaa wandani wa Dkt Ruto eneo hilo wamejaribu kutishwa kwa kupokonywa walinzi majuzi lakini hawakurudi nyuma, bado wakizidisha uhusiano.

Swali kuu sasa ni ikiwa kuzidi kuchelewa kwa Rais na mabwanyenye wa eneo hilo kutangaza mrithi wa Rais atakayekuwa msemaji wa Mlima Kenya kutagharimu eneo hilo kisiasa katika uchaguzi ujao, na kumnufaisha Naibu Rais ambaye haachilii nafasi yoyote kupiga siasa huko.

You can share this post!

JAMVI: Muthama afufua uhasama wake na Mutua kuhusu dai la...

JAMVI: Sababu kuu za pwani kulemewa kujibunia chama kimoja...

adminleo